Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa anaiwekea vikwazo vikali Iran ikiwemo afisi ya kioingozi mkuu wa dini Ali Khamenei.

Bwana Trump amesema kuwa vikwazo hivyo vya ziada ni kujibu hatua ya Iran kuiangusha ndege isio na rubani ya Marekani na mambo 'mengine mengi'.

Ayatollah Khamenei , ambaye ndio kiongozi mkuu nchini Iran alilengwa kwa kuwa ndiye anayehusika na hali ya uhasama katika utawala wa taifa hilo.


Waziri wa maswala ya kigeni nchini humo Mohamed Javd Zarif alisema kuwa Marekani haipendelei diplomasia.

Katika ujumbe wa Twitter kufuatia tangazo la rais Trump, bwana Zarif pia aliushutumu utawala wa Trump kwa kuwa na kiu ya vita

Hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili imekuwa ikipanda katika wiki za hivi karibuni.

Hatahivyo waziri wa fedha nchini Marekani Steve Mnuchin alisema kuwa maagizo ya rais Trump ambayo yatazuia mabilioni ya madola ya mali ya Iran yalikuwa yanaandaliwa hata kabla ya Iran kuiangusha ndege ya Marekani isiokuwa na rubani katika Ghuba wiki iliopita.

Je ni nani anayeathiriwa?

Wizara ya fedha nchini Marekani imesema kuwa makomanda wanane wa Iran ambao husimamia kitengo kinachoshauri vitendo vya jeshi kuu la {Islamic Revolution Guard Corps} IRGC walikuwa wanalengwa katika vikwazo hivyo vipya.

Iliongezea kuwa agizo la rais Trump pia litaunyima uongozi wa Iran kupata raslimali za kifedha mbali na kuwalenga watu walioajiriwa na kiongozi huyo wa dini katika afisi kadhaa ama nyadhfa tofauti mbali na taasisi za kigeni za kifedha ambazo huwasaidia kufanya biashara.

Marekani imedai kwamba Ayatollah Khamenei ana utajiri mkubwa ambao unafadhili jeshi la IRGC.

Mwaka 2018 waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo alisema kwamba kiongozi huyo ana utajiri wenye thamani ya $95b ambao hutumika kulifadhili jeshi hilo.