Sudan imezuwiliwa kushiriki katika shughuli zote za Umoja wa Afrika kufuatia uvamizi wa kijeshi dhidi ya waandamanaji mapema wiki hii, uliopelekea vifo vya zaidi ya watu 100. Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetangaza hayo hapo jana.


Taifa hilo litazuwiliwa kushiriki katika harakati zote za Umoja wa Afrika hadi utawala wa mpito utakaoongozwa na raia utakapoanzishwa. “Hiyo ndio njia pekee ya kuikwamua Sudan kutoka mzozo unaoendeelea”, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa Twitter.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Deutsche Welle (DW), Uamuzi huo umepitishwa baada ya vikosi vya usalama vya Sudan kuwafyetulia risasi wanaharakati waliokuwa wakiandamana kwa amani Jumatatu iliyopita mjini Khartoum-dazeni kadhaa ya watu wameuwawa.

Hapo awali wizara ya afya ilikanusha ripoti kwamba vikosi vya usalama vimewauwa waandamanaji wasiopungua 100 na kusema waliouliwa hawakupindukia watu 46. Kamati kuu ya madaktari wa Sudan inasema watu wasiopungua 100 wameuwawa ikiwa ni pamoja na maiti 40 za watu zilioopolewa kutoka Mto Nile.