MAMBO vipi mpenzi msomaji wangu wa safu hii ya Staa na Familia, kama ilivyo ada ya safu hii ni kuwasaka mastaa mbalimbali na kuelezea maisha yao halisi wanayoishi na watoto wao pamoja.Leo tunaye mwanamuziki wa miondoko ya mduara, Snura Mushi ambaye amejaaliwa kuzaa watoto wawili wa kike na wa kiume lakini wote hakubahatika kukaa na baba zao, yeye kama yeye anahangaika nao kwa kila kitu kuanzia kula mpaka mavazi na hapa chini anafunguka maisha anayoishi na watoto zake hao:Wikienda: Msomaji angependa kujua we’ ni mama wa aina gani kwa watoto wako?

Snura: Ni mama ambaye ninapenda sana kusikiliza watoto wangu, naona kama ndugu zangu wa karibu kwa sababu kuna wakati unaweza kuongea nao hata mipango ya maisha japo ni wadogo.

Wikienda: Maisha ya kuwalea watoto wako bila baba unayachukuliaje?Snura: Ni mabaya mno tena sana, kwa sababu kila unachokifanya unajua uko wewe kama wewe, hakuna msaada kutoka popote pale na pia huna mtu wa karibu wa kuzungumza naye kuhusiana na mtoto, lakini kubwa watoto wanapata mapenzi ya upande mmoja tu, huku wanaona watoto wengine wana baba zao.Wikienda: Sasa unawezaje kuwalea kwa kuwahudumia kila kitu.

Snura: Naweza, nafanya kazi kwa ajili yao na kila kitu nafanya nikijua ninao mbele yangu, yaani mimi ndio nimebeba maisha yao yote.

Wikienda: Ni kitu gani ambacho hupendi kuona kwa watoto wako?Snura: Kwanza sipendi kuona hawana furaha hata kidogo, sipendi kuona nyuso zao hazina matumaini na pia sipendi kuona wanasononeka kwa chochote kile.

Wikienda: Sasa watoto hawakuulizi kuhusu baba zao?

Snura: Unajua watoto wana akili sana, wanajua kila kitu wanaelewa baba zao wapo lakini hawajali kitu juu yao.Wikienda: Kutokana na kazi yako ya sanaa inakubidi kusafiri huku na kule je, inakuaje kuhusu watoto?

Snura: Watoto wangu hawana shida na mmoja yupo shule ya bweni, mwingine yupo na hata nikiondoka kuna watu sahihi wa kuwaangalia.

Wikienda: Unataka watoto wako wajifunze nini?Snura: Napenda sana watoto wangu wamjue Mungu, wajue kusali na waishi katika imani thabiti.

Wikienda: Ungependa watoto wako warithi kazi yako?

Snura: Hapana, ndio maana nafanya kazi na kuhangaika kwa ajili yao kwa sababu nataka wapate elimu bora na wafanye kazi waipendayo maana mimi mama yao sikupata bahati ya kusoma.

Wikienda: Asante sana Snura.

Snura: Karibu.