BAADA ya juzi Jumatano kusambaa taarifa zinazomuhusu kiungo wa Simba, James Kotei kutimkia katika Klabu ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini, aliyewahi kuwa kocha wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema Simba wamefanya makosa kumuachia mchezaji huyo.



Kotei aliyejiunga na Simba, Desemba 2016 ametwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA mara moja huku akiisaidia Simba kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.



Akizungumza na Championi Ijumaa, Julio alisema kitendo cha Simba kumuacha mchezaji huyo ni kosa kubwa ambalo watalijutia kwa muda mrefu kwa kuwa kiungo huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji wanaofanya kazi kwa ufasaha akiwa dimbani.



“Simba wamekosea sana kumuacha Kotei, sielewi maamuzi hayo kayafanya nani, hauwezi kumuacha mchezaji kama Kotei ambaye kila mmoja alikuwa anajua kazi yake akiwa uwanjani.



“Mimi naamini pengo la Kotei litawaumiza na watakuja kujutia uamuzi wao, hauwezi kumuacha mtu ambaye ameshaifahamu Simba na kutegemea watu ambao hauna uhakika kama watapafomu, sijui pale Simba kuna kitu gani,” alisema Julio.