HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imevipatia vikundi 71 vya wanawake, vijana na walemavu, sh230.8 milioni ya mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuwanyanyua kiuchumi.

Ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Asia Ngalisoni akizungumza jana alisema vikundi hivyo ni vya kata 14 vilivyonufaika na mkopo huo.

Ngalisoni alisema mkopo huo umenufaisha vikundi 71, ambapo 59 ni vya wanawake 1,531, vikundi tisa vya vijana 238 na vikundi vitatu vya walemavu 57.

Alisema hadi mwezi Mei mwaka huu halmashauri hiyo imekusanya sh1.7 bilioni ikiwemo mapato ya ndani na marejesho ya fedha za vikundi vilivyokopeshwa awali.

"Mfuko huu unawanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi vyenye shughuli za ujasiriamali au vinavyokusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati," alisema Ngalisoni.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema fedha hizo zinazotolewa hazina riba hivyo vikundi hivyo vinapaswa kuchukua mikopo hiyo na kurejesha kiasi kile kile walichokopa.

"Nitoe wito kwa vikundi vyote vilivyokopeshwa na halmashauri virejeshe fedha hizo kwa wakati ili wengine nao waweze kukopa na kujikwamua kiuchumi," alisema Chaula.

"Mfuko huu unawanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi vyenye shughuli za ujasiriamali au kinakusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati," alisema Chaula.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck alimpongeza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri yake Yefred Myenzi kwa kusimamia ipasavyo mapato hadi kufanikisha utolewaji wa mikopo hiyo.

"Wakati halmashauri nyingine zikisuasua kufanikisha mikopo sisi Simanjiro tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani tunatoa mikopo hadi fedha nyingine zimebaki," alisema Sipitieck.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi alitoa wito kwa vijana wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo kwani mwitikio wao bado ni mdogo.

"Zile fedha zenu vijana za asilimia nne mnazopaswa kupewa hamjazichukua hivyo vijana wa Simanjiro mnapaswa kubadilika ili mnufaike kupitia mikopo hii tunayoitoa," alisema Myenzi.

Katibu wa walemavu mji mdogo wa Mirerani, William Orata alisema kupitia mkopo waliopata wamefanikisha uanzishwaji wa mashine ya kusaga nafaka.

Mmoja kati ya wanawake walionufaika na mkopo huo, Susan Alanyamuna alisema wameweza kutengeneza sabuni aina ya Sidai.
 Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) akipokea mfano wa hundi kutoka benki ya NMB.
 Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) akipeana mkono na viongozi wa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu baada ya kupokea mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Wilaya hiyo
 Baadhi ya vikundi vya wajasiriamali, wanawake, vijana na walemavu waliopatiwa mkopo wa sh 230.8 milioni na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.