Kuanzia tarehe 30 Mei, 2019 kuna taarifa zilizosambaa na kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu mama mjamzito anayesemekana kujijeruhi maeneo ya tumboni na kupelekea kutoa mtoto tumboni,tukio lililotokea katika kata ya Kirando Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.


Baada ya kupokea taarifa hizo timu ya ufuatiliaji iliyoundwa na wataalam wa Afya kutoka ngazi ya Mkoa na Wilaya husika ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa ilifanya ufuatiliaji wa tukio hilo kwa lengo la kupata uhalisia wake na kubaini mambo yafuatayo:

1. Mhusika katika tukio hili ni Bi Joyce Mweupe Kalinda mwenye umri wa miaka 32 anayeishi katika Kitongoji cha Kalya, Kijiji cha Kamwanda, Kata ya Kirando, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa, umbali wa takribani kilometa moja kutoka Kituo cha  Afya Kirando.

 2.Bi Joyce alipokelewa katika kituo cha Afya Kirando kilichopo katika kata ya kirando Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi majira ya saa 09:30 alfajiri ya tarehe 30 Mei 2019 akiwa amesindikizwa na ndugu zake wawili (Wifi na Shangazi yake) kwa lengo la kujifungua ambapo alipokelewa na kufanyiwa uchunguzi wa awali.

Katika uchunguzi huo ilibainika kuwa mama huyo alikuwa na
ujauzito unaokadiriwa kuwa na miezi tisa, akiwa na dalili za
uchungu katika hali ya kawaida kiafya.

4. Baada ya uchunguzi wa awali kukamilika alipelekwa katika wodi ya wazazi wanaosubiri kujifungua kwa ajili ya kupumzika huku watoa  huduma wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wengine.

5. Katika ujauzito huu alikuwa akihudhuria kliniki ya Afya ya Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya Kirando ambapo alifanikiwa kufanya mahudhurio matatu na hudhurio la mwisho likiwa ni tarehe 08 Mei, 2019

6. Mnamo saa 10:30 alfajiri wakati watoa huduma wakifuatilia kujua maendeleo yake ndipo walipobaini kuwa Bi Joyce hakuwepo ndani ya wodi na hivyo kuanza kumtafuta katika maeneo mbalimbali ya kituo cha afya na kutoa taarifa kwa mlinzi na uongozi wa kituo cha afya.

7. Wakati juhudi za kumtafuta zikiendelea, majira ya saa 12:30 asubuhi Bi Joyce aliletwa kituoni akiwa amebebwa kwenye godoro na watu watatu (Mojawapo akiwa ni mwenyekiti wa Kijiji cha Kamwanda) huku akivuja damu nyingi.

8. Watoa huduma walimpokea mgonjwa na kumuona akiwa ametapakaa damu, mtoto akiwa nje ya tumbo. Baada ya kumchunguza Bi Joyce alibainika kuwa na jeraha lilililosababishwa na kitu chenye ncha kali tumboni huku sehemu ya utumbo, mfuko wa uzazi, kondo la nyuma na mtoto vikiwa nje na yeye mwenyewe akiwa hajitambui. Baada ya hapo timu ya Kituo cha Afya ikongozwa na Mganga Mfawidhi Dkt. Gideon Msaki iliendelea na huduma za upasuaji wa dharura kwa ajili ya kuokoa Maisha ya Bi Joyce.

Baada ya huduma za upasuaji wa dharura kufanyika timu ya ufuatiliaji iliendelea na ufuatiliaji zaidi wa tukio hili na kubaini ifuatavyo:

1. Bi Joyce alipotoka kituo cha Afya alirudi nyumbani kwake anapoishi yeye,mtoto wake wa kiume aitwaye Linus Sindani anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 12 au 13 na mume wake ambaye siku ya tukio hakuwepo nyumbani. 2. Mara baada ya kurudi nyumbani Bi Joyce alimwagiza mwanaye (Linusi) kwenda kumuita shangazi yake ambaye anaishi maeneo ya jirani na nyumbani kwao. Waliporudi wakiwa na shangazi ndipo walipomkuta Bi Joyce akiwa ameloa damu na hivyo kutoa taarifa kwa majirani na mwenyekiti wa Kijiji kwa ajili ya msaada
zaidi.

Hitimisho
1. Timu ya ufuatiliaji imejiridhisha kuwa huduma za dharura za upasuaji wa kuokoa Maisha ya Bi Joyce zimefanyika kwa mafanikio makubwa katika kituo cha Afya Kirando na kwamba mama na mtoto ambao kwa sasa wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa uangalizi zaidi wanaendelea vizuri

2. Tunatoa pongezi kubwa kwa watumishi wa Kituo cha Afya Kirando kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa Maisha ya Bi Joyce Kalinda.

3. Tukio hili limeripotiwa katika jeshi la Polisi kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi zaidi.