*Dkt. Kalemani aeleza kuwa shilingi bilioni 64 zimetengwa kwa ajili ya marekebisho kwa maeneo yanayokatika umeme kuanzia Julai mwaka huu

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa  sekta ya nishati nchini imeimarika zaidi kuanzia mwaka 2015 hadi sasa ambapo idadi ya viwanda, wateja na upelekaji wa umeme vijijini umeimarika kwa kasi zaidi na hiyo yote ni kutokana na kasi ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli hasa kwa kuweka mikakati mizuri kwa wenye viwanda.

Akizungumza wakati wa kikao kilichokutanisha wizara ya nishati na jumuiya ya wamiliki wa viwanda nchini Dkt. Kalemani amesema kuwa kikao hicho kimelenga kusikiliza na kutatua kero na changamoto za wenye viwanda na kueleza kuwa ili sekta ya viwanda iendelee lazima wadau wahusishwe na hiyo ni mara ya nne kwa wadau kukutana.

Kalemani amesema kuwa uwepo wa nishati ya uhakika kumepelekea viwanda kuongezeka kutoka viwanda 2800 mwaka 2015 hadi zaidi ya viwanda zaidi ya 5200 mwaka huu huku wateja wa nishati ya umeme wakiongezeka kutoka milioni 1.4 hadi wateja milioni 2.45.

Kuhusiana na upelekaji wa umeme vijijini waziri Kalemani amesema kuwa vijiji  zaidi ya 7600 ambavyo ni sawa na asilimia 72 vimepata umeme  ukilinganisha na vijiji 1208 vilivyopata umeme kwa mwaka 2015 na kueleza kuwa hadi kufikia mwaka 2020 asilimia 85 ya wakazi wa vijijini watakuwa wamefikiwa na huduma ya umeme.

Aidha Kalemani amesema kuwa serikali ina mipango ya kutosha ya kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ambapo takribani shilingi bilioni 64 zimetengwa, kujengwa kwa transifoma katika maeneo mbalimbali pamoja na uwekaji wa miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo na nyaya ardhini mpango utakaoanza mwakani jijini Dodoma na baadaye jijini Dar es Salaam.

Vilevile Kalemani amewahakikishia wawekezaji pamoja na wenye viwanda uhakika wa soko na nishati na kusema kuwa serikali ipo nao sambamba na amezitaka mamlaka husika kutoa huduma kwa ufanisi pamoja na kuweka mazingira bora kwa wawekezaji kwa kuzingatia huduma ya umeme inakua imara, toshelevu, inayotabirika na yenye gharama nafuu.

Kwa upande wake mwenyekiti  wa taasisi ya sekta binafsi nchini (TPSF) Salum Shamte amesema kuwa serikali iangalie namna ya kutoa vipaumbele vya fursa kwa wazawa ili kuweza kujenga taifa la viwanda.

Shamte amesema kuwa wazawa wapewe fursa katika kujenga miundombinu ya aina hiyo ili kuokoa fedha na kujenga mabilionea wengi zaidi.

Aidha ameiomba mamlaka husika kutoa gesi kwa sekta binafsi ili waweze kusambaza majumbani pamoja na kuzalisha umeme.

Mkutano huo umehudhuriwa na wamiliki wa viwanda, mameneja wa TANESCO nchi nzima kikanda pamoja na watendaji wa sekta ya nishati.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na jumuiya ya wenye viwanda nchini kwenye mkutano uliowakutanisha ambapo wamejadili kero,  na utatuzi wa changamoto hizo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa taasisi ya sekta binafsi nchini (TPSF) Salum Shamnte akizungumza wakati mkutano huo ambapo ameiomba serikali kutoa gesi kwa sekta binafsi ili waweze kuzalisha umeme na kusambaza gesi majumbani,  jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI) Frank Daffa akitoa salama katika mkutano huo ambapo ameiomba mamlaka husika kuangalia suala la ukatikaji wa umeme hasa katika maeneo ya uzalishaji,  jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Waziri wa Nishati na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.