Mshambuliaji wa Manchester United Romelu Lukaku ''anapaswa kuondoka'' kwenye klabu hiyo, ameeleza kocha wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez.

Lukaku, 26, alijiunga na United akitokea Everton kwa kitita cha pauni milioni 75 mwezi Julai mwaka 2017 na ameifungia magoli 42 katika michezo 96.

Mchezaji huyo alihusishwa na mipango ya kuondoka Old Trafford msimu huu wa joto baada ya kuwa na wakati mgumu chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

''Ni muhimu sasa kwa Rumelu kutafuta klabu inayofaa,''Martinez ameliambia gazeti la Ubelgiji, Het Laatste Nieuws.

Martinez,ambaye alimfundisha Lukaku akiwa Everton na sasa katika timu ya taifa, ameongeza: ''Ni wazi kuwa anapaswa kuondoka Manchester United.''

Lukaku ambaye alikua akihusishwa na taarifa za kuhamia Inter Milan, mkataba wake na United utakamilika mwaka 2022.

Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya baadae baada ya ushindi wa 3-0 wa Ubelgiji dhidi ya Scotland na kufuzu michuano ya Euro ya 2020 juma lililopita, alisema: ''Nitajua nitakachofanya, lakini sitasema.Tutaona.''

Alifunga magoli 15 katika michezo 45 msimu uliopita lakini Solskjaer amekua akipendelea zaidi kumtumia mshambuliaji Marcus Rashford.