Jeshi la Polisi mkoani Tabora limefanikiwa kuanza kuudhibiti mtandao wa wizi wa vyuma vya kingo za barabarani baada ya kuwakamata watu watano akiwemo mmoja mkazi wa Singida ambaye anatajwa kuwa ni mhalifu mzoefu anayejihusisha na wizi wa vyuma hivyo katika mikoa ya Simiyu, Singida na Tabora.

Mtuhumiwa huyo pia anafahamika kwa kwa jina maarufu la Mtipa na wenzake wamekamatwa na kikosi kazi kutoka Ofisi ya Afisa Upelelezi wa Mkoa wa Tabora wakiwa huko mkoani Singida wakijiandaa kwenda kuiba vyuma vingine kwenye Barabara mpya ya Mwigumbi huko mkoani Simiyu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Emmanuel Nley amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kudai kuwa kikosi kazi hicho kiliwakamata watu hao watano wakiwa tayari na vyuma hivyo aina ya ‘Guard Rail’ walivyovifungua katika Barabara za Nzega - Tabora na Nyahua - Tabora ambavyo walikwenda kuviuza kwa wakandarasi wengine. Vyuma hivyo vinadaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 62.