Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameagiza kuwafutia leseni wafanyabiashara wa madini, wanaotumia leseni moja ya madini kufanya biashara ukoo mzima.
Aidha, ameshangazwa na watu wachache wenye mtandao wa kuiba madini, wakitorosha madini nchini na kwenda nchi jirani ya Kenya.
Mshangao huo wa Biteko aliupata jana baada ya kusafiri alfajiri na kuwasili mkoani Arusha, kujionea madini ya tanzanite na mengineyo yakiwa yamekamatwa yakiwa na thamani ya Sh milioni 958.
Biteko ameyasema hayo kwa masikitiko akiwa Benki Kuu (BoT) tawi la Mkoa wa Arusha, alipofika kujionea madini hayo yaliyohifadhiwa ndani ya sanduku maalumu la kuhifadhi nyaraka za serikali, yakiwa katika vifurushi tofauti tofauti.
Aliongeza kuwa katika tukio hilo, kuna watu nyuma yake, na wote waliohusika watachukuliwa hatua zinazostahili.
Amesema anashindwa kuelewa wachimbaji wanahitaji nini wakati serikali imewafutia kodi na kufungua soko la madini siku 12 zilizopita, ambalo limeiingizia serikali zaidi ya Sh bilioni 2.5.
"Naagiza askari waliokamata madini haya kupewa shilingi milioni tano na shilingi milioni tano nyingine kwa mtoa siri aliyesaidia madini hayo kukamatwa," alisema Biteko.