Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, inawachunguza askari polisi sita wa Kituo cha Igunga kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh. milioni 8.

Polisi hao wanadaiwa kuomba kiasi hicho kutoka kwa mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa, Ngaka Mataluma (95) ili wasimpeleke kituoni.

Inadaiwa kuwa Juni 12, mwaka huu, askari hao walikwenda kwa Mataluma na kuomba Sh milioni 20, lakini wakajadiliana hadi Sh milioni 8.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley, alikiri kuwapo tukio hilo na kusisitiza kuwa wenye nafasi ya kulizungumzia vizuri ni Takukuru ambao ndio wanahusika zaidi na masuala ya rushwa.

“Suala hili nimelisikia, wenzetu wa Takukuru ndio wanaohusika zaidi na masuala ya rushwa, watafuteni, sisi tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwao, tutachukua hatua,” alisema Kamanda Nley.

Alipotafutwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Chaulo Mussa alisema wako hatua za mwisho za kukamilisha upelelezi wa suala hilo.

“Ni kweli tukio hili lipo, tupo hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi wetu, baada ya hapo tutatoa majibu,” alisema.

Diwani wa Kata ya Isakamaliwa, Dotto Kwilasa (CCM) alisema baada kutokea tukio hilo, aliamua kuitisha mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na wananchi zaidi ya 680.

Alisema katika mkutano huo, wananchi walitoa malalamiko dhidi ya askari hao sita na viongozi wa Serikali wawili.

Askari hao ni  Inspekta Frank Matiku, PC Raphael Maloji, D.1 Koplo Paul Bushishi, PC Lome Laizer, DC Lucas Nyoni na Koplo Charles ambao wote wanafanya kazi Kituo cha Polisi Igunga.

Viongozi wa Serikali ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isakamaliwa, Edward Kitenya na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zahanati, Maulid Hamisi