SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema wabunge 48 watakwenda kuishangilia timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazofanyika nchini Misri wakiambatana na Peter Mollel maarufu kama Pierre Konki Liquid.

Pierre  ni mmoja wa wachekeshaji wakubwa nchini.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Juni 18, 2019 Ndugai amesema wataambatana na mchekeshaji huyo katika fainali hizo huku akiwataka wabunge zaidi kujiandikisha ili kwenda Misri.“Hizi fainali ni muhimu na ninawashauri wabunge ambao hawajajiandikisha wafanye hivyo ili tukaishangilie timu yetu na kutembelea maeneo mbalimbali huko Misri,” amesema Ndugai.

Wiki iliyopita Ndugai alisema wabunge wanaotaka kukaa siku nne Misri wanatakiwa kulipia Dola 720 za Marekani (sawa na Sh1.7 milioni), wanaotaka kukaa siku 10 watapaswa kulipia Dola 1,490 (sawa na Sh3.5 milioni).

Katika fainali hizo zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19, 2019, Taifa Stars imepangwa kundi moja na Algeria, Senegal na Kenya.