Inaarifiwa kuwa Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) zimeungua moto usiku wa kuamkia leo na kusababisha vitu vilivyokuwamo ndani kuungua moto.

Polisi mkoani Lindi imesema imeanza uchunguzi wa kubaini chanzo cha ofisi hizo kuchomwa moto.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Proudencia Protus amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema uchunguzi unafanywa ili kubaini chanzo chake.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Cecil Mwambe amesema mali zilizochomwa ni pamoja na pikipiki mpya iliyokuwa ipelekwe wilayani Liwale kwa ajili ya shughuli za chama, kompyuta na nyaraka mbalimbali na kwamba taarifa zimeshatolewa polisi.

“Ni taarifa za kweli ofisi iliyopo Lindi mjini imechomwa moto usiku wa kuamkia leo muda wa saa nane usiku, ndani kulikuwa na pikipiki mpya ambayo ilikuwa ipelekwe Liwale kwa ajili ya zoezi la Chadema ni msingi, kompyuta ya chama na nyaraka mbalimbali. Taarifa imeshafikishwa polisi, hii ni baada ya zoezi la Chadema ni msingi kupamba moto,” amesema Mwambe.

Mmoja wanachama wa chama wa chama hicho, Juma Mwinga amesema ilikuwa majira ya saa nane usiku wakati tukio hilo linatokea baada ya jirani kusikia harufu ya moshi.