Mwanamke mmoja raia wa Tanzania alikamatwa wikendi iliopita kufuatia madai ya mauaji ya jirani yake kutoka Kenya katika eneo la Chhattapur kusini mwa jimbo la Delhi kufuatia mgogoro kati yao kuhusu chupa ya pombe.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania mtuhumiwa amedaiwa kuwa mkaazi wa jiji la Dar es salaam.

Maafisa wa polisi wanasema kwamba mwili wa marehemu uliopatikana nyumbani kwake ulikuwa na majereha ya kisu kifuani.


Wakati wa uchunguzi, watu kadhaa raia wa Kenya na Watanzania pamoja na wale wa Nigeria walihojiwa na maafisa wa polisi.

"Tulipokea simu mwendo wa saa mbili na dakika kumi usiku kutoka kwa mwanamke mmoja raia wa Kenya akidai kwamba dadake ameuwawa'', alisema kamishna wa polisi wa wilaya ya kusini Vijay Kumar akinukuliwa na gazeti la The Nation nchini Kenya baada ya kuzungumza na gazeti la India Express nchini humo.

"Tulikimbia katika eneo la mkasa na kumpeleka mwanamke huyo hospitalini ambapo daktari alisema kwamba tayari alikuwa amefariki."

Rekodi za mawasiliano ya simu na kanda za video za CCT zilitathminiwa ambapo mtuhumiwa ambaye alikuwa akiishi katika nyumba moja ilio mkabala na jumba ambalo marehemu alikua akiishi alikamatwa kulingana na naibu huyo wa kamishna wa polisi .

Akihojiwa na polisi mtuhumiwa aliambia maafisa hao kwamba sku mbili zilizopita alikuwa amemtaka marehemu kumpatia pombe swala ambalo alikataa.

Ni wakati huo ambapo walirushiana maneno kabla ya mshukiwa kumdunga kisu marehemu, alisema afisa huyo wa polisi wa eneo la Delhi.

Kisu pamoja na nguo ambazo mshukiwa huyo alikuwa amevaa wakati wa kisa hicho zilipatikana nyumbani kwake.

Kulingana na gazeti la Nation nchini Kenya, mtuhumiwa na mpenzi waake walikua katika nyumba hiyo wakati wa mgogoro huo.

Gazeti hilo limedai kwamba wawili hao walitoroka lakini walipatikana na kushirikishwa katika uchunguzi , afisa aliyekuwa akifanya uchunguzi huo aliambia gazeti la Hindustan Times

Mwanamume huyo alikiri kwamba mpenzi wake alikosana na marehemu kuhusu chupa ya pombe.