Na John Nditi
UTAFITI wa Teknolojia ya Uhandisi Jeni ( GMO) katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo Makutupora na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI ), Mikocheni unaendelea na utakapokamilika matokeo yake yatawasilishwa serikalini kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi ya kuitumia au kitoitumia.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Tafiti za bioteknolojia za kilimo nchini, Dkt. Fredy Tairo kutoka Taasisi ya Utafiti ya TARI Mikocheni wakati akiwasilisha mada ya hali ya utafiti wa GMO nchini kwenye mkutano wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini.

Mkutano wa mjadala huo uliofanyika Chuo Kikuu Dar es Salaam na kuandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya Chuo Kikuu hicho.

Dk, Tairo alisema, msimamo wa Serikali ni kuendelea Utafiti wa GMOs ili uweze kukamilika katika hatua zake muhimu na kisha utakapokamilika katika hatua zote utapeleka katika Mamlaka husika kwa ajili ya kutoa maamuzi hapa nchini.

Alisema, watu na baadhi ya vyombo vya habari walielewa vibaya kauli iliyotolewa na serikali ilitaka watafiti wafuate utaratibu wa kutoa matokeo waliyokuwa wanayapata kwenye majaribio hayo ili kuondoa mkanganyiko.

Mratibu huyo wa Bioteknolojia katika mada yake alisema , sababu na umuhimu wa serikali kufanya tafiti za GMO ili kukabiliana na Changamoto sugu zinazotokana na madiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame, wadudu na magonjwa sugu ili kuongeza tija kwa wakulima.

Amesema, kuwa majaribio yanayofanyika katika taasisi ya utafiti ya Makutupora Mkoani Dodoma unalenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya ukame na bungua wa mahindi na kwa matokeo ya awali yameonyesha kufanikiwa pia kupambana pia na Viwavi jeshi vamizi.

Kwa upande wa utafiti wa zao la Muhogo unaofanyika katika Taasisi ya utafiti ya TARI Mikocheni alisema ,unalenga kuipa kinga mihogo kupambana na magonjwa sugu ya Batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo yanaathiri zao hilo Afrika hasa kusini mwa Jangwa la Sahara.

Naye Mtafiti kutoka Chuo kikuu cha Sayansi na teknolojia cha Nelson Mandela , Mashamba Philipo alisema , teknolojia hiyo ni nzuri na kwa serikali,wakulima na Watafiti ni kuona kama ni muda muafaka wa teknolojia hiyo kutumika hapa nchini.

Mtafiti huyo (plant breeder) alisema, teknolojia hiyo ina uwezo wa kuwezesha nyanya kuwekewa jeni ambayo inauwezo wa kuifanya isiharibike ndani ya mwezi mmoja hata baada ya kuichuma na hivyo kumuongezea tija mkulima.

“Hii sio teknolojia ngeni duniani maana nchi za Marekani, China, Brazil na nyingine nyingi za Afrika zinaitumia , lakini ni muhimu wadau wote wapewe elimu ili kuondoa mashaka waliyonayo kuhusu teknolojia hii” alisema Mtafiti Philipo.

Naye Mratibu wa tafiti za Bioteknolojia nchini, Dk Raphael Nduguru alisema ,walizunguka nchini nzima na kukusanya mbegu za asili na kuanzia utafiti na kuongeza jeni ili kuweza kukabilina na magonjwa yanayohusiana na mihogo.

Naye Mtafiti Emmanuel Sulle ambaye ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Western Cape Afrika Kusini alisema , kuna haja ya Serikali ya Tanzania kuongeza bajeti kwenye tafiti za kilimo nchini ili kuwezesha watafiti wa ndani kupatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima.

Alisema , mbali na fedha lakini iongeze idadi ya watafiti kwenye aina ya utafiti huo ambao unakuwa kwa kasi Duniani ili waweze kuwa na uwezo wa kufanya tafiti hizo katika viwango vinavyotakiwa kimataifa.

Sulle alisema , licha ya kufanya tafiti za GMO lazima watafiti waangalie na pia na mbinu zingine za asili wanazozitumia wakulima na kuziboresha. 
 Mratibu wa Tafiti za Bioteknolojia katika kilimo kutoka TARI Mikocheni , Dk. Fredy Tairo akizungumza na na waandishi wa habari wakati wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini na kuandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.


 Baadhi ya Washiriki kutoka idara, taasisi, mashirika na wadau wengine wa kilimo wakifuatilia mada wakati wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini na kuandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Mratibu wa Tafiti za Bioteknolojia katika kilimo kutoka TARI Mikocheni , Dk. Fredy Tairo ( Kulia) , pamoja na Profesa Daudi Mukangara ( kati kati ) wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) ambaye alikuwa ni Mwongoza mada pamoja na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela ,Mashamba Philipo ( kushoto) wakisilikiza hoja mbalimbali ziliozolewa kwenye mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini ulioandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.