Mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola amewekwa kizuini katika Hospitali ya Kericho, eneo la Bonde la Ufa kusini-magharibi mwa Kenya.

Mgonjwa huyo, ambaye ni mwanamke anaripotiwa kuwa na dalili zinazowapata wagonjwa wa Ebola.

Maafisa wa afya katika Kaunti ya Kericho wamesema kuwa alifanya safari kutoka Malaba eneo la mpaka kati ya Kenya na Uganda.

Hakuna ripoti yeyote iliyotolewa ya kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola karibu na mpaka wa Malaba:Isipokuwa eneo la Magaharibi mwa Uganda.

Sampuli za damu za mgonjwa huyo zimechukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.

Mgonjwa huyo alikwenda hospitali binafsi siku ya Jumapili alikua na homa,maumivu ya kichwa,maumivu ya viungo,maumivu ya koo na alikua akitapika.

Alitibiwa malaria kwenye hospitali ndogo lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya .

Alifanyiwa tena kipimo cha malaria na majibu yalionyesha hana malaria.Kutokana na hali hiyo wahudumu wa afya walimpa rufaa kwenda hospitali ya Kaunti ya Kericho ambayo ina uwezo wa kuweka karantini.


Matokeo ya awali ya vipimo yanatarajiwa kuwa tayari katika kipindi cha saa 12 mpaka 24.

Idara ya huduma za afya ya kaunti ya Kericho imesema inafuatilia kwa karibu suala hili na inafanya kazi pamoja na serikali kuu kuhakikisha kuwa hatua madhubuti zinafuatwa kuhakikisha usalama wa kiafya kwa wengine.

Serikali ya Kaunti imeuhakikishia Umma kuwa hospitali ya kaunti ina uwezo na ina vifaa kuhakikisha mgonjwa anatengwa na kuwalinda watumiaji wengine wa hospitali na imetoa wito kwa watu kuwa watulivu na wenye subira.

Ebola Uganda

Juma lililopita Mtoto wa miaka mitano nchini Uganda alipatikana kuwa na Ebola, shirika la afya duniani (WHO) lilithibitisha.

Uthibitisho kwamba ni ugonjwa wa Ebola ulitolewa na taasisi ya kupambana na virusi nchini Uganda Virus Institute (UVRI) Jumanne juma lililopita baada ya kutangazwa rasmi na maafisa.

Wizara ya afya nchini Uganda na WHO walituma kikosi maalum kutambua wengine walio katika hatari, taarifa ya pamoja ilieleza.

Waziri wa afya Uganda Jane Ruth Aceng aliwaambia waandishi wa habari kwamba familia ya mtoto huyo inaangaliwa, wakiwemo wawili walioonyesha kuwa na dalili za kama za ugonjwa wa Ebola.

Baada ya hapo alituma ujumbe kwenye Twitter akieleza kwamba nchi hiyo imeingia katika 'hali ya muitikio'kufuatia kisa hicho.

Taarifa za baadae zilisema kuwa mtoto huyo alipoteza maisha

Tayari wahudumu 4, 700 nchini Uganda wamepewa chanjo dhidi ya ugonjwa huo, taarifa hiyo ya pamoja ya Shirika la afya duniani na wizara ya afya nchini Uganda ilithibitisha.

Tahadhari Tanzania

Watanzania wametakiwa "wasiwe na hofu" kuhusu kusambaa kwa Ebola. Waziri wa afya Ummy Mwalimu alisema baada ya taarifa za Ebola kuingia Uganda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.