Vikosi vya ulinzi nchini Sudan vimetumia nguvu kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliokita kambi nje ya makao makuu ya jeshi jijini Khartoum.

Kwa mujibu wa waandamanaji hao, milio ya risasi imekuwa ikisikika na tayari watu kadhaa wameripotiwa kujeruhiwa kwenye rabsha hizo.

Sudan imekuwa chini ya utawala wa Baraza la Kijeshi la Mpito toka Rais Omar al-Bashir alipinduliwa mwezi Aprili.

Waandamanaji wamekuwa wakilazimisha utawala urejeshwe mikononi mwa serikali ya kiraia.

Ramadhan 'inavyoimarisha' maandamano Sudan
Mazungumzo ya mzozo wa Sudan yakwama
Jeshi la Sudan laafiki kipindi cha mpito cha miaka mitatu
"Kwa sasa kuna jaribio la kutawanya waandamanaji waliokita kambi," imeeleza taarifa fupi kutoka kwa Jumuiya ya Wataalamu wa Sudani amabo ndio waratibu wa maandamano hayo ya kitaifa.

Mashuhuda wanasema kuwa kwa sasa waandamanaji wanachoma matairi na kuweka vizingiti ili kuwazuia maafisa usalama kuwafikia.

Inaripotiwa kuwa mtu mmoja amepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Mwanahabari Benjamin Strick, ambaye amebobea katika kusanifisha picha zinazotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, ametuma video kadhaa za kile kinachoendelea kwa sasa katika jijila Khartoum.

Hakimiliki ya Picha @BenDoBrown@BENDOBROWN
Jeshi la Sudani mpaka sasa bado lipo kimya juu ya kinachoendelea.

Waandamanaji wamekita kambi mbele ya makao makuu ya jeshi toka Aprili 6 mwaka huu, siku tano kabla ya Bashir kupinduliwa na jeshi.

Mwezi uliopita, viongozi wa waandamanaji na majenerali wa jeshi walitangaza kuwa wamefikia muafaka wa muundo wa serikali ya mpito ya miaka mitatu ambayo itaandaa uchaguzi wa kiraia.

Lakini wamesema bado wanatakiwa kufanya maamuzi ya nani aingie kwenye baraza huru ambalo ndilo litakuwa na maamuzi ya mwisho kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitatu.

Hapajaweza kufikiwa makubaliano juu ya upande upi baina ya raia na wanajeshi uwe na wawikilishi wengi kwenye baraza hilo.