Mkazi wa Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam Mirajdin Tajdin (32), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya  kusafirisha dhahabu bila kuwa na kibali.



Tajdin ambaye ni mkazi wa Mtoni  Mtongani amefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi, Juni 20, 2019 na kusomewa mashtaka na wakili wa Serikali Ester Martin.

Martine amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 50/ 2019.

Akimsomea hati ya mashtaka, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Janeth Mtega, Wakili Martin amedai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo April 30, 2019 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere( JNIA) uliopo  wilaya ya Ilala.

Amedai siku hiyo ya tukio, mshtakiwa  alikutwa na vipande vya dhahabu vyenye uzito wa gramu 98, vikiwa na thamani ya dola za Marekani 3636.92, sawa na Sh 8, 364,914 Mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la  pili, muda na eneo hilo, Tajdin anadaiwa kusafirisha dhahabu hiyo bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka husika.