Leo ni siku ambayo mbivu na mbichi zitafahamika baada ya michezo ya marudio ya mchujo wa kupata timu mbili zitakazopanda Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu ujao.

Timu za ligi kuu, Kagera Sugar na Mwadui FC zitatoa timu moja ambayo itayosalia katika ligi baada ya dakika 90, huku timu za daraja la kwanza, Pamba FC na Geita FC pia zikigombe nafasi moja.

Kagera Sugar leo itakuwa kibaruani kucheza mchezo wa pili dhidi ya Pamba katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, huku Mwadui FC ikimenyana na Geita FC uwanja wa Mwadui mjini Shinyanga.

Katika michezo ya awali, timu zote mbili zina kumbukumbu ya kutoka suluhu kwenye mechi zao, hivyo leo ni lazima washindi wawili wapatikane ili kutimiza idadi ya timu 20 zitakazocheza ligi kuu msimu ujao .

Kama Mwadui na Kagera zitapoteza mchezo wa leo basi itakuwa fursa kwa Pamba na Geita kupanda chati na kupata nafasi ya kushiriki ligi kuu.