Baadhi ya kampuni au mashirika yanayofanya kazi hapa nchini (Tanzania) yana kampuni zake tanzu au mama nje ya nchi. Hili kimsingi halina ubaya. Ubaya unakuja pale ambapo kampuni hizo tanzu au kampuni mama; zinapotumika kufanya udanganyifu wa kukwepa kodi, tozo, malipo ya mrahaba pamoja na gawio. *Na udanganyifu huo mara nyingi hufanyika kwa kuongeza gharama za uendeshaji ili kupunguza kiwango cha faida ambacho kampuni zilizopo hapa nchini zinapata; ama zinaonekane zinapata hasara*. Ujanja huu kwa kitaalamu unaitwa *transfer pricing*.

Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo hayo, mbinu mojawapo inayotumika ni katika ununuzi wa mitambo na vipuri. Ili kupandisha gharama za uendeshaji, kampuni za hapa nchini huagiza vifaa hivyo kupitia kampuni tanzu au mama zilizopo nje ili Serikali isifahamu gharama halisi*. Kampuni hizo tanzu zikishanunua vifaa hivyo huviuza kwa kampuni za hapa nchini kwa bei ya juu; wakati mwingine mara tano zaidi ya bei halisi. Na kwa vile sheria zetu za kodi na uwekezaji zinatoa misamaha ya kodi, gharama hizi za kununua vifaa zinaendelea kukatwa katika mapato ya kampuni hizo miaka nenda miaka rudi; na hivyo kuzifanya kampuni hizo zisilipe kabisa ama zilipe kiwango kidogo sana cha kodi na tozo mbalimbali.

Wataalaamu hao wanabainishwa kwamba njia nyingine inayotumika ni kupitia mikopo. Kampuni za hapa nchini huchukua mikopo kwa riba kubwa kutoka kwenye kampuni zao tanzu au mama zilizopo nje ya nchi*. Hii inaongeza gharama za uendeshaji na kuzifanya kampuni za hapa nchini kila wakati zionekane zinajiendesha kwa hasara na hivyo kuzifanya zisilipe kodi. Lakini, cha kushangaza ni kwamba, licha ya kupata hasara, makampuni hayo yanaendelea kufanya kazi.

Wamesema pia kwamba mbinu nyingine inayotumika na makampuni kukwepa kutoa gawio au kulipa kodi na tozo mbalimbali, ni kupitia gharama za usimamizi (yaani management fee)*. Kampuni hizi hulipa menejimenti zao gharama kubwa; na wakati mwingine huajiri kampuni nyingine kuzisimamia kampuni zao. Hii inapandisha gharama za uendeshaji na kuzifanya kampuni husika zionekane zinapata hasara kila kukicha na hivyo zishindwe kulipa kodi na tozo nyingine.