Familia ya Baba wa Taifa imezungumzia afya ya Mama Maria Nyerere aliyeugua ghafla akiwa Kampala nchini Uganda kabla juzi kuwasili nchini na kulazwa.

Akizungumza msemaji wa familia hiyo, Makongoro Nyerere, alisema mama yake aliugua ghafla akiwa Kampala na baadaye alipowasili nchini alipumzishwa.

Alisema alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam, akitokea Kampala alikokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.

“Sukari ya mama ilipanda ghafla na kulazimika kupelekwa hospitali ambako baada ya uchunguzi madaktari walimruhusu asafiri kuja Dar es Salaam baada ya afya yake kuimarika kidogo.

“Alipowasili nchini alipumzishwa kwa muda wakati madaktari wakiendelea na uchunguzi kabla ya kufikia uamuzi wa kumlaza, lakini tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema Makongoro.

Mke huyo wa Mwalimu Nyerere, alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe ya ibada maalumu ya kumbukumbu ya mashahidi wa Uganda eneo la Namugongo iliyofanyika Juni 3, mwaka huu.

Baada ya mjane huyo wa Baba wa Taifa kuugua, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alishindwa kuhudhuria sherehe hizo na kwenda kumtembelea hospitalini.