Wakazi wa Maai Mahiu mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya wamepigwa na bumbuwazi baada ya mwanamke mmoja kuushona mdomo wa mtoto wake wa kiume anayesoma darasa la tano kwa sababu ya kushuka kimasomo.Gazeti la Daily Nation nchini Kenya limeripoti.

Tukio hilo la Jumamosi liliwaacha majirani midomo wazi kwa kutoamini kilichotokea.

Mkazi mmoja alisema mwanamke huyo anayefanya kazi kwenye saluni ya urembo, aliumizwa na maendeleo ya mtoto wake shuleni yaliyokuwa yameshuka.

Katika kumuadhibu, Mama alimshona mdomo mtoto wake kwa kutumia sindano kabla ya majirani kuingilia kati.

Kamishna msaidizi wa Kaunti hiyo, Julius Nyaga, ameiambia Daily Nation kuwa taarifa za tukio hilo zimemfikia.
Tukio hilo limeelezwa kuwa la kikatili na Polisi wanamsaka mshukiwa.

''Polisi wanamtafuta Mama wa mtoto baada ya uongozi wa shule kuripoti kwenye mamlaka,'' Alisema bwana Nyaga.

Amewataka wazazi kuacha kuwafanyia vitendo vya kikatili watoto, akiwaasa kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Badala yake Nyaga amesema ni vyema kwa wazazi kutafuta masaada wa kitaalamu kuwasaidia watoto badala ya kuchukua hatua kali zinazosukumwa na hasira.