Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, mhe. Paul
Makonda ametangaza kuwa siku ya Jumamosi, Juni 22 ni siku ya maombi kwa mkoa wake kwaajili ya Taifa Stars.

Amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mkutano ambao ulihudhuriwa na Waziri wa Habri, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dr. Harrison Mwakyembe.

RC Makonda amesema, "siku ya Jumamosi, Juni 22, 2019 itakuwa ni siku ya maombi ya mkoa wa Dar es Salaam kuiombea Taifa Stars. Naomba tuungane na wanamichezo wote kwa sababu Jumapili Stars ndio inacheza na Senegal".

"Moja ya jambo ambalo mimi naliamini ni maombi, naomba mpenzi na mkereketwa wa michezo Jumamosi tuungane kwenye ulimwengu wa roho kuiombea Stars. Maandalizi yapo, nguvu ya pesa ipo lakini mkono wa Mungu hauepukiki kwenye ushindi, wengine huita bahati lakini tukimuomba Mungu atatupa majibu sahihi kwamba Tanzania itapata mafanikio makubwa", ameongeza Makonda.

Kwa upande wake Waziri Mwakyembe amezindua kampeni ya kuichangia Taifa Stars ambayo amesema itaendelea hadi Alhamisi, Juni 20, ambapo itafanyika hafla maalumu itakayohudhuriwa na viongozi wa serikali.