Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba imesema hakuna mtu atakayekamatwa kwa kukutwa na vifungashio vya vyakula mfano wa karanga, Ubuyu, kwani kinachokatazwa ni kutumia vifungashio hivyo kubebea bidhaa nyingine.


Kauli hiyo ameitoa siku moja baada ya kusambaa habari kuwa Serikali imepiga marufuku matumizi ya vifungashio vinavyohifadhia vyakula kama ubuyu, karanga, ice cream.

“Vifungashio vya bidhaa za vyakula (karanga, ubuyu, etc) havijaxwwzuiwa. Kinachozuiwa ni vi-plastic hivi transparent ambavyo huwa vinafungia karanga, ubuyu etc visitumike kuendea sokoni/dukani kubebea bidhaa. Hakuna mtu atakamatwa kwa kuuza karanga kwenye kifungashio cha plastiki” ameeleza waziri Makamba katika mtandao wa Twitter kuwaeleza wananchi.

Hata hivyo, Makamba ameeleza kuwa zipo bidhaa ambazo lazima zifungwe kwenye mifuko ya Plastiki ili kulinda ubora wa bidhaa hizo kama magodoro, peremende na biskuti hivyo bidhaa kama hizo zitaendelea kuwa kwenye mfumo huo wa kufungwa kwenye vifungashio vya Plastiki.