Huko mkoani Mbeya ni majonzi ya msiba mzito wa ndugu wanne wa familia moja akiwemo Bibi Harusi Mtarajiwa Diana, wote wamefariki juzi kwenye ajali ya gari wakitoka Mbeya kuelekea Dar es salaam harusini, maziko yao wote yamefanyika nyumbani kwao Mbeya kijiji cha Majengo kata ya Chimala.Bwana harusi Elisante ambaye ndiye alikuwa afunge ndoa na Diana kesho, alionekana kukosa nguvu za kuhimili kushiriki shughuli kutokana na uchungu wa kuondokewa na mke mtarajiwa.

Wakati anaaga miili hiyo, Elisante ameonekana kuishiwa nguvu na kudondoka chini kabla ya kusaidiwa na vijana wawili waliokuwa wakimshikiria muda wote baada ya kuiona sura ya mkewe mtarajiwa (Diana).

Ajali hiyo ilitokea juzi alfajiri barabara Kuu ya Mbeya-Makambako baada ya gari walilokuwa wakisafiria wanafamilia sita kutoka nyumbani kwao Chimala wilayani Mbarali kuelekea Dar es Salaam kugongwa kwa nyuma na lori aina Fuso na kusababisha vifo vya watu wanne na wawili kujeruhiwa. Gari hiyo baada ya kugongwa na Fuso ilitumbukia mtaroni na kupinduka.

Watu waliofariki dunia ni Diana Mwandunga ambaye alikuwa bibi harusi mtarajiwa, Faraja Mwandunga, James Mwandunga na mtoto wa Faraja, Jacton (2) wakati waliojeruhiwa ni Ibrahimu Mwandunga na Nico Mwandunga.