Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa inaungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya kwa lengo la kuikumbusha jamii juu ya tatizo kubwa lilipo katika jamii yetu juu ya Biashara na Matumizi ya Dawa za hizo.

Kitaifa Maadhimisho haya kwa mwaka huu yatafanyika jijini Tanga siku ya Jumatano tarehe 26 mwezi Juni, 2019 katika viwanja vya Tangamano na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa George H. Mkuchika (Mb).

Kauli mbiu ya Kimataifa ya maadhimisho haya kwa mwaka huu inasema Waathirika wa Dawa za Kulevya Wana Haki ya Kupata Huduma za Afya. Kwa kuzingatia Kauli mbiu hii inakumbusha kuwa mapambano dhidi ya Tatizo la Dawa za Kulevya yanahitaji mikakati mtambuka na jumuishi ikiwemo suala la tiba kwa waathirika. 

Ni muhimu kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya kupata tiba stahiki na zilizothibitishwa kisayansi (evidence based practices) ili kuweza kupunguza madhara ya dawa hizo kwa waraibu na jamii inayowazunguka. Baada ya tiba hizo, huduma endelevu za Stadi za Kazi pamoja na Ushauri Nasaha kuzingatiwa ili kuwasaidia waathirika wasirudi kwenye matumizi ya dawa za kulevya. 

Aidha, mkakati huu unaenda sambamba na mkakati wa utoaji wa elimu kwa vijana ili wasiingie kwenye matumizi ya Dawa za Kulevya pamoja na Udhibiti wa wafanyabiashara wa Dawa hizo.

Maadhimisho haya ni fursa kwa umma wa Watanzania kwa vile Tatizo la Dawa za Kulevya linaathiri nchi yetu katika nyanja za kiafya, kijamii, kiuchumi pamoja na kutishia ulinzi na usalama wa nchi yetu. Katika maadhimisho haya Watanzania wataweza kupata elimu na kukumbushwa kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana athari kubwa kwa mtumiaji, kwa jamii na kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Tatizo la dawa za kulevya husababisha madhara kiafya ikiwa ni pamoja na kuchochea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI, virusi vya homa ya ini aina ya B na C, Kifua Kikuu, magonjwa ya akili, pamoja na usugu wa tiba ya kifua kikuu na UKIMWI. Aidha, baadhi ya dawa za kulevya husababisha matatizo ya uzazi ikiwemo upungufu wa nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo ya akili pamoja na kuenea kwa kansa mbalimbali kama vile kansa ya koo, mapafu na mara nyingine husababisha vifo ghafla vya kutokana na dozi kuwa kubwa “overdose”. 

 Aidha Serikali imeendelea kusimamia utoaji tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo, na kufanikiwa kuongeza idadi ya waathirika wa dawa za kulevya katika vituo vya tiba kutoka wagonjwa 2,400 mwaka 2015 hadi wagonjwa 7000 mwaka 2018. Hali hii imeasaidia kupunguza maambukizi ya UKIMWI kwa waraibu wa dawa za kulevya wanaojidunga kutoka 35% mwaka 2015 hadi 18.5%.

Pia, Serikali inamtaka kila mwananchi kwa nafasi yake katika jamii kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa endapo kutabainika kuwepo kwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Pamoja na hilo Serikali inatoa wito kwa viongozi wa dini kulikemea suala la matumizi ya dawa za kulevya misikitikini na makanisani. 

Sambamba na hilo, Serikali inawakumbusha Viongozi wa dini zote kuwa wana nafasi kubwa katika jamii ya kuhakikisha watoto, vijana pamoja na jamii yote kwa ujumla wanapata mafunzo ya kuwajenga kiroho, kimwili na kisaikolojia ili wawe na tabia njema katika jamii na mfano wa kuigwa kwa matendo mema.

Serikali inaikumbusha jamii kushiriki kikamilifu katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, kujenga malezi bora kwa watoto katika ngazi ya familia, na kuwapeleka kwenye matibabu watumiaji wa dawa za kulevya. Vilevile, Serikali inasisitiza Jamii kuzitambua, kuzienzi na kuziendeleza tamaduni zetu nzuri ili kuinusuru Wananchi wote hasa vijana ambao ndo nguvu kazi ya taifa na matumizi ya dawa za kulevya.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMANNE, JUNI 25, 2019