Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameipongeza timu ya Taifa Stars kwa kuitangaza nchi kimataifa licha ya matokeo kuwa sio mazuri kwenye michuano ya AFCON inayoendelea nchini Misri.


Waziri Kigwangalla ametoa pongezi hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kusema kuwa “Watu wangu wa nguvu, msiumie, msisononeke. Mmetupa heshima, mmetufikisha juu sana. Matokeo ni kitu kingine, mmeitangaza nchi yetu parefu sana. Safari na iendelee.”.

Kwa upande mwingine, Waziri Kigwangalla amewapa ofa wachezaji wote wa Taifa Stars kutembelea hifadhi za taifa kwa ajili ya mapumziko pindi watakaporudi nchini.

“Kumbukeni mna offer yangu ya kwenda kupumzika kwenye hifadhi zetu. Kazi kwenu kuitumia” ameandika Waziri Kigwangalla.

Jana Taifa Stars ilipoteza mchezo wake wa pili wa AFCON 2019 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya. Matokeo ambayo yameifanya Tanzania kutolewa kwenye michuano hiyo licha ya kubakiza mchezo mmoja dhidi ya Algeria.