Ikiwa leo michuano ya Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 ndio inaanza kutimua vumbi nchini Misri, mataifa 24 yatakayoshiriki mtanange huo yameonywa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwamba yajiandae kwa mashindano yatakayochezewa kwenye joto kali.

Taarifa kutoka nchini Misri ambako mashindano haya yatafanyika kuanzia leo Juni 21 hadi Julai 19 zinasema kwamba Kamati ya mashindano inayojihusisha na masuala ya afya kwenye CAF imeitisha mapumziko ya lazima ya dakika tatu baada ya dakika 30 za kwanza na pia itakapogonga dakika ya 75, mbali na yale ya kawaida ya dakika 15 kipindi cha kwanza kinapomalizika.

Mashindano haya makubwa barani Afrika yalihamishwa kutoka tarehe zake za kawaida za Januari na Februari hadi Juni na Julai kwa mara ya kwanza kutokana na mivutano kati ya klabu na nchi. Hali ya joto nchini Misri wakati huu inatarajiwa kufikia kati ya nyuzi joto 35 na 38.