Kulikuwa na hali ya mshtuko katika mahakama moja mjini Eldoret siku ya Jumanne baada ya kubainika kuwa mshukiwa aliyekuwa akishikiliwa kwenye gereza la wanawake ni mwanaume.
Mshukiwa huyo anayetambulika kwa jina Shieys Chepkosgei siku ya Jumatatu alikamatwa katika Chuo na Hospitali ya Rufaa ya Moi ambapo alikua akifanya kazi kama muuguzi mwanafunzi wa kike ingawa hakusajiliwa hapo.
Baada ya kushtakiwa, alipelekwa kwenye gereza la wanawake la Eldoret kusubiri maamuzi ya mahakama huku akitambuliwa kama mwanamke.Gazeti la Daily Nation la Kenya limeripoti.
Hatahivyo, siku ya Jumanne askari magereza katika ukaguzi wao wa kawaida waligundua kuwa mshukiwa alikua mwanaume.
Uchunguzi wa haraka ulifanyika kubaini ukweli kabla ya kufanyiwa vipimo ili kujihakikishia jinsia yake.
Hakimu wa mahakama hiyo Charles Obulutsa siku ya Jumanne alilazimika kutoa amri nyingine ikielekeza kuwa mshukiwa ashikiliwe kwenye kituo cha polisi cha Eldoret Magharibi ili kutoa nafasi ya kufanyika uchunguzi wa kitabibu kuthibitisha jinsia yake.
Miondoko ya fasheni yatikisa jela Brazil
Morsi azikwa saa chache baada ya kifo
Hakimu Obulutsa alichukua hatua hiyo baada ya ofisa mkuu wa gereza la wanawake la Eldoret kutaka mahakama irejee amri yake akielezea kuwa mshukiwa ashikiliwe kama mfungwa wa kiume
Katika kesi hiyo mahakama ilielezwa kuwa tarehe 14 mwezi June mshukiwa huyo akiwa na nia ya kufanya udanganyifu, mshukiwa alijifanya kuwa mwanafunzi wa kike wa taaluma ya uuguzi kwa jina Pamela Mulupi.
Awali, Hakimu Obulutsa aliamuru mtuhumiwa ashikiliwe gerezani mpaka tarehe 24 mwezi Juni, Gazeti la Daily Nation limeripoti.
Shauri hilo litatajwa tena tarehe 27 mwezi Juni