Leo ni siku ya bajeti kwa nchi za Afrika Mashariki, ambapo mawaziri wa fedha wa nchi hizo watawasilisha bajeti za serikali za nchi zao kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Serikali ya Tanzania inapanga kutumia takriban $14.3 bilioni, katika mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni ongezeko , kutoka shilingi trilioni 32.5 za Kitanzania katika mwaka wa fedha 2017/2018.

Waziri wa fedha Philip Mpango, amesema sehemu kubwa ya makadirio hayo ya fedha katika bajeti zitatumika katika kuimarisha miundo mbinu ikiwemo reli barabara na kusambaza umeme katika maeneo ya vijijini.

Bajeti ya Kenya, inakadiriwa kuwa dola bilioni 30.2, ambayo ni kubwa kuliko bajeti zote za nchi zingine za afrika mashariki kwa pamoja.

Uganda kwa upande wake inakadiria bajeti ya dola bilioni 10.9 huku Rwanda dola bilioni 3.17.

Bajeti ya Kenya zaidi ya Tanzania, Rwanda na Uganda pamoja

Kwa upande wa Uganda, wakosoaji wanaiona nchi hiyo ikiendelea kutingwa na madeni, nakisi ya biashara na kuongezeka kwa kiwango cha umasikini.

Hata hivyo viongozi wa serikali ya nchi hiyo wanapinga na kueleza uchumi wa nchi hiyo ni imara na unaendelea kukua.

Deni la Kenya limezidi utajiri wake kwa 57%, sehemu kubwa ikitokana na wakopeshaji na wawekezaji wa kimataifa.

Kwa upande mwingine takwimu za madeni ya Rwanda, na Tanzania ni chini ya 40% ya pato jumla nchini.

Huku mapato yakishuka katika mataifa yote ya Afrika mashariki, inatazamiwa kwamba awamu nyingine ya malipo ya kodi na mikopo yataidhinishwa na mawaziri wa fedha katika bajeti ya mwaka huu.

Ina maana gani kwako?
Swali kubwa linaloulizwa ni Bajeti hizi zina maana gani kwa raia wa kawaida?

Hii ni fursa ya kuelewa serikali imelenga nini katika ugavi wa rasilmali na pia kusaidia kutathmini uzito inayoweka katika masuala ya maendeleo yanayomgusa na kumfaidi mwananchi.

Bajeti hizi pia zinatoa ufafanuzi wa iwapo umaskini unapungua katika mataifa.

Wafadhili wasitisha ufadhili kwa bajeti ya Tanzania
Ripoti ya CAG yabainisha hali mbaya ya kifedha kwa mashirika ya Umma Tanzania
Kipimo kinatokana na kuangalia iwapo mahitaji ya raia masikini yanazingatiwa kwa rasilmali za serikali au iwapo kodi zinazoidhinishwa zinawalemaza zaidi masikini.

BBC Swahili imezungumza na baadhi kuhusu matarajio yao katika bajeti ya mwaka huu Afrika mashariki: