WaKaTi leo (Jumatatu) aliyekuwa mfanyabiashara bilionea bongo, Dk reginald abraham Mengi, akitimiza siku 40 tangu afariki dunia, mjane wake Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’ amefuguka kuhusu kipindi hiki cha msiba wa mumewe, Ijumaa Wikienda linaye.K-Lynn kupitia kwa rafiki yake wa karibu ambaye hakutaka kuandikwa jina gazetini aliliambia Ijumaa Wikienda juzi (Jumamosi) lililotaka kujua mjane huyo ana kauli gani kwa Watazania baada ya aliyekuwa mumewe kulala mauti kwa muda wa mwezi mmoja na siku kumi hadi sasa ambapo alisema;“Hakuna jambo kubwa sana alilonalo Jack Mengi (K-Lynn) katika kipindi hiki kizito cha majonzi kama shukrani kwa ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa jumla.

“Hata kama ningekupa simu uongee naye (K- Lynn) angekuambia haya ninayokueleza, kikubwa anawashukuru wote walioshirikiana naye katika wakati huu wa maombolezo ya msiba wa mumewe,” alisema rafiki huyo wa karibu.40 ITAFANYIKAJE?

Kwa kawaida jamii nyingi Bongo huichukuliwa siku ya arobaini tangu marehemu kufariki kuwa ni ya kuondoa msiba ambapo sala au dua za kumuombea marehemu na sadaka mbalimbali hutolewa kwa ajili yake.Kufuatia utaratibu huo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta kwa njia ya simu ya mkononi Wakili Michael Ngalo ambaye wakati wa msiba alikuwa mtoa taarifa ili kujua machache yatakayofanyika siku ya 40 ya mfanyabiashara huyo ambayo ni leo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Hata hivyo, baadhi ya ndugu walipotafutwa walisita kuzungumzia chochote kuhusu siku hiyo.K-LYNN AANDIKA WARAKA

Katika hatua nyingine siku chache kabla ya kuifikia siku ya arobaini ya mumewe, K-Lynn aliandika waraka kwa lugha ya Kingereza kupitia ukurasa wake wa Instagram uliobeba ujumbe wa shukrani kwa wote waliokuwa nyuma ya familia yao wakati wa msiba.Sehemu ya waraka huo ilisomeka hivi; “May God bless all of your kind hearts who continue to pray for us, we can never thank you enough or repay you for your kindness.” Kwa tafsiri isiyo rasmi waraka huo ulimaanisha; “Mungu awabariki kwa mioyo yenu mnaoendelea kutuombea, hatuwezi kushukuru kwa kutosheleza au kulipa wema wenu.”

MASTAA WAMTIA MOYO K-LYNN

Baada ya kuandika waraka huo, maneno yake yaliwagusa wengi ambapo baadhi ya mastaa Bongo walijitokeza na kumtia moyo kwa kuweka komenti zao kwenye ujumbe huo wa shukrani aliouandika mjane huyo wa Mengi.Miongoni mwao ni mtangazaji Zamaradi Mketema ambaye alimtaka K-Lynn kuendelea kuwa na ujasiri wa kukabili changamoto za msiba huku Flora Lauwo akiweka mikono yenye alama ya shukrani na alama ya moyo wa

upendo. Mlimbwende Miriam Odemba yeye alimtaka mjane huyo kuendelea kuwa na nguvu huku mtangazaji Maimartha Jesse akimshukuru kwa waraka wake na wengine wengi nao wakitoa shukrani na kuonesha upendo kupitia alama na maneno mafupi.


NDUGU WA MENGI WASHAURIWA

Wakizugumza na Ijumaa Wikienda jijini Dar katika mahojiano maalum, baadhi ya wananchi hasa wenye maisha ya nchini waliishauri familia ya mzee Mengi kuwa makini katika kuenzi na kulinda heshima ya mfanyabiashara huyo aliyekuwa kipenzi cha watu.“Mimi ninachowaomba ndugu wa marehemu, waache mambo ya Kiswahili ya kugombea mali na kuvurugana, watunze heshima ya baba yao. “Mzee huyo anatakiwa kuenziwa kwa sababu ni mfano wa kuigwa kwa kizazi na kizazi,” alisema Sulemani Mkono, mkazi wa Temeke ambaye ni mlemavu wa macho.Naye Alfred Charles wa Mwananyamala Kwa Kopa alisema; “Litakuwa jambo zuri kama itatengwa siku maalum kila mwaka ya kuwaenzi watu kama Mengi ambao wametoa michango yao kwenye taifa hili na kuinua wengine kimaisha, jambo hili litasaidia kujenga jamii inayosaidiana.”TUJIKUMBUSHE

Mengi alifariki dunia Dubai katika Nchi za Falme za Kiarabu Mei 2, mwaka huu na kuzikwa Mei 9, nyumbani kwao Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro.Mengi anatajwa kuacha utajiri unaokadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.2 ambapo inaelezwa kuwa, katika maisha yake alitumia fedha zake kusaidia watu wengine hasa walemavu na maskini ili kuwawezesha nao kuishi maisha ya furaha.