BAADA ya taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo, kuhusu hali ya beki wa timu ya Simba na  ya Taifa Stars, Shomari Kapombe,  kwamba amejitonesha majeraha yake,  Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ameibuka na kuhoji kuhusu ukweli wa jambo hilo.

Ndimbo alisema kuwa wachezaji wa Stars wameanza mazoezi kwa muda wa wiki moja kabla ya kwenda nchini Misri kwa michuano ya Afcon na  kwamba Kapombe amejitonesha sehemu aliyokuwa ameumia.

“Mchezaji Kapombe amejitonesha wakati akifanya mazoezi na wachezaji wenzake, hivyo hatafanya tena mazoezi na wenzake mpaka pale hali yake iakapotengamaa,” alisema Ndimbo awali.

Lakini, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Manara alihoji ni nani alitoa taarifa hiyo na ni wapi aliumia mchezaji huyo wa Simba wakati aliachiwa programu na kocha.

“Ni wapi taarifa za kuumia au kujitonesha kwa Kapombe zimetokea?   Kapombe anayo program maalum anayoifuata kwa sasa na wala hajajitonesha kokote kule, na kiukweli amesikitishwa na hizo taarifa zinazozagaa katika mitandao ya kijamii.

“Nimeongea naye na ameniomba niwaombe Wana-Simba na Watanzania wazipuuze taarifa hizo zisizokuwa na chanzo na Inshaallah Mungu atamponya kiraka huyu mwenye mapafu makubwa na ufundi wa kutosha,” amesema.

Kapombe amesema  alikuwa akifanya mazoezi binafsi kutokana na programu ambayo ameachiwa na kocha wa timu ya Simba.

“Nimepewa programu maalumu na kocha wa Simba, ambayo itachukua muda kidogo, hivyo baada ya kuitwa timu ya taifa niliwasilisha ‘proposal’ yangu kwa timu hiyo ili wajue ukweli na wao wawe na maamuzi juu yangu kwa kuwa nilikuwa nina muda maalumu ambao sikutakiwa kugusa uwanja.

“Nimepigiwa simu na watu wangu wa nyumbani wakiwa wamepoteza furaha, wakiniuliza kwa nini sijawaambia kama nimeumia tena? Imeniumiza sana kwani hakuna ukweli wowote mimi naendelea na mazoezi na sina tatizo lolote zaidi ya kuendelea na mazoezi niliyopewa na kocha wangu wa Simba, nipo vema na ninaendelea salama,” amesema Kapombe.