Msaidizi na Mshauri Mkuu wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Iran, Yahya Rahim Safavi amesema kuwa meli zote za Marekani katika Ghuba ya Uajemi, ziko katika shabaha ya makombora ya nchi kavu kuelekea baharini ya majeshi ya wanamaji ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC.)

Meja Jenerali Safavi ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la FARS ambapo sambamba na kuashiria kwamba Wamarekani wana zaidi ya vituo 25 vya kijeshi katika eneo lote la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ameongeza kwamba Washington inafahamu vyema kwamba meli zao zote katika eneo la Ghuba ya Uajemi ziko katika shabaha ya makombora hayo ya jeshi la IRGC.

Akibainisha kwamba shambulizi moja tu katika Ghuba ya Uajemi litapandisha bei ya mafuta kufikia dola 100 kwa pipa, amebainisha kwamba kupanda huko kwa bei ya mafuta kutazifanya Marekani, Ulaya na hata washirika wa Marekani kama vile Japan na Korea Kusini, zishindwe kuvumilia.