Iran "imefanya kosa kubwa sana" kwa kuitungua ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani, ameeleza Rais Donald Trump.

Hata hivyo Trump amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo yawezekana lilisababishwa na makosa ya kibinaadamu.

"Ni vigumu sana kwangu kuamini kwamba tukio hilo lilikuwa la makusudi," amesema Trump.

Iran inasema ndege hiyo ya kijasusui ilikuwa ndani ya anga lake, lakini jeshi la marekani limekanusha na kusema ilikuwa ikipaa katika anga la kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Javad Zarif amesema nchi yake itapeleka malalamiko Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Marekani inavamia eneo lake.

Balozi wa Iran wa UN Majid Takht Ravanchi amesema ni dhahiri kuwa ndege hiyo ilikuwa inafanya operesheni ya kijasusi wakati ikitunguliwa, kitu ambacho amesema ni uvunjifu wa wazi wa sheria za kimataifa.

Katika barua aliyomuandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Bw Ravanchi amesema, Japo Iran haitaki kuingia vitani, lakini ina haki ya kujilinda dhidi ya vitisho vya maadui.

Trump amesema nini?
Akizungumza kutokea Ikulu ya White House, amesema kuna ushahidi kuwa ndege hiyo ilikuwa katika anga la kimataifa na si eneo la Iran.

"Nafikiri, huenda Iran ilifanya kosa - Yawezekana kuna jenerali ama mtu mwengine ambaye alifanya kosa hilo la kutungua ndege ile," amesema.

"Yawezekana alikuwa ni mtu mmoja mpuuzi (ndio alitoa amri ya kutungua)."