Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) nchini Tanzania, Simon Sirro amewatoa hofu wananchi juu ya tishio la ugaidi katika maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam.

IGP Sirro amesema taarifa hizo zimeshaanza kufanyiwa kazi huku akisema jeshi lake lilishapata fununu za shambulio hilo kabla Ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari juu ya tukio hilo kupitia tovuti yake Juni 18, 2019.

IGP Sirro amesema, “hiyo ni taarifa kama taarifa nyingine, inaweza kuwa ya kweli au uongo, lakini sisi kama vyombo vya ulinzi huwa hatupuuzi jambo. Tangu jana tulipata hiyo taarifa kwa hiyo tuko vizuri, timu zetu za operesheni na intelijensia na wengine tunaifanyia kazi,” Sirro alieleza wakati akizungumzia taarifa hiyo ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

Katika tangazo lake Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania inaeleza kuwapo kwa uvumi wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika eneo la Masaki hususani hoteli za kitalii na maduka ya maeneo hayo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi.