KISMATI! Ukiona hadi staa mwenzako anakupa heshima, jua unachofanya ni kikubwa! Nahodha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Cameroon, Klabu ya Barcelona na Chelsea, Samuel Eto’o amempigia saluti staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ au ‘Mondi’ siku chache baada ya kualikwa nyumbani kwake. Kwa mujibu wa chanzo, Mondi ndiye aliyeanza kumfuata Eto’o nyumbani kwake nchini Ufaransa hivi karibuni ambapo inadaiwa alikuwa katika pilikapilika za kutengeneza video.

“Ujue kwa kipindi kirefu Mondi alikuwa nchini Ufaransa na madansa wake pamoja na meneja wake, Sallam SK akitengeneza video yake ya Inama aliyomshirikisha Fally Ipupa. “Alipokuwa nchini humo alipata nafasi ya kwenda kumtembelea Eto’o nyumbani kwake,” kilisema chanzo na kuongeza;

AONESHWA MAKOMBE

“Baada ya kufika akiwa na Sallam walipewa misosi ya nguvu na mwisho wa siku akaoneshwa makombe yake tofauti ikiwa ni sehemu ya mafanikio yake tangu ameanza soka.“Makombe hayo yalikuwa ni pamoja na matatu ya UEFA aliyoyapata akiwa na vilabu tofauti.”

MONDI ALIPA

Hata hivyo, Mondi alitumia mwanya huo kumkaribisha Eto’o nyumbani kwake, Mbezi-Beach jijini Dar baada ya kusikia amealikwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano maalum ya mpira wa miguu. “Wakiwa Mbezi-Beach, Mondi alihakikisha Eto’o anakula vyakula vya Kibongo na mwisho wa siku naye akampeleka kuangalia mafanikio yake kwenye muziki ambapo alimuonesha tuzo zake nyingi zilizopangwa kwenye kabati maalum ambazo alizipata ndani na nje ya nchi kwa nyakati tofauti.

“Baada ya yote kupita, Mondi alimsikilizisha baadhi ya nyimbo zake na mwisho kabisa wakaelekea eneo la kucheza pool table na kuanza kucheza,” kiliweka nukta chanzo hicho.

ETO’O AMPIGIA SALUTI

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Eto’o aliweka picha aliyopiga na Mondi na kuandika; “Kutoka Paris (Ufaransa) hadi Dodoma (alichanganya kidogo alikuwa akimaanisha Dar es Salaam). Asante sana kwa kunipatia chakula usiku wa jana.

“Najisikia faraja kuwa na kaka wanaofanya vitu vya tofauti Afrika. Ubarikiwe kwa huduma yako nzuri.” Mondi naye aliingia katika komenti hiyo na kujibu; “Kaka natumaini umependa chakula cha Kibongo.”