NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA 

HALMASHAURI ya Mji Kibaha ,Mkoani Pwani inajenga soko kubwa, la kisasa kwenye eneo la kitovu cha Mji 
litakalogharimu takribani sh.bilioni 7.3. 

Fedha hizo za ujenzi huo ni kati ya kiasi cha sh.bilioni 8 zilizotolewa na serikali inayoongozwa na Rais wa awamu ya tano Dr.John Pombe Magufuli ambazo zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi mkakati ya halmashauri mbalimbali ambapo Kibaha mji imezielekeza katika mradi wa soko la kisasa  

Ofisa mawasiliano ,habari na uhusiano wa halmashauri ya Mji huo, Innocent Byarugaba ,aliwaambia waandishi wa habari kwamba, soko hilo litakuwa na ghorofa moja, linatarajiwa kukamilika mwezi disemba, 2019. 

Aidha alieleza, miundombinu mingine itakayokuwepo ni vyumba vya maduka 43, benki mbili, ATM 12, maegesho ya magari ya kawaida 150, malori ya mizigo 15, uzio wenye urefu wa mita 
565.4, tangi la chini ya ardhi la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kuweka lita 110,000. 

Byarugaba alimtaja, mkandarasi aliyepewa tenda ni kampuni ya Elerai ya Jijini Arusha. “Tulikuwa hatuna soko la kisasa, tunaishukuru sana serikali kwa kuidhinisha kiasi hicho cha fedha” 

“Kwani usanifu umefanyika itatumika bilioni 7.3 kwa kujenga soko hilo kubwa huko karibu kabisa na stendi ya kisasa katika kitovu cha mji wetu ,”alifafanua Byarugaba. 

Pamoja na hayo, ofisa habari huyo alieleza ,halmashauri ya Mji imeanza pia ujenzi wa machinjio ya kisasa eneo la Mtakuja itakayogharimu sh.bilioni 1,968,505,115″:, fedha hizi ni ufadhili kutoka benki ya dunia kupitia mfuko wa uboreshaji na uendelezaji miiji (ULGSP).