Baada ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kutoa taarifa katika mtandao wao wa kijamii wa “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama “security alert” hapo jana Juni 19, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umemwita wizarani Kaimu Balozi wa Marekani ili kutoa ufafanuzi wa “twitter” yao hiyo.

Angalizo hilo la kiusalama lilitokana na uvumi uliodaiwa na ubalozi huo kusambaa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika kuitikia wito huo, Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani, Janine S. Young alifika wizarani hapo na kuonana na uongozi wa wizara hiyo uliomtaka kueleza sababu za kutoa taarifa hiyo bila kushirikisha mamlaka husika.

Janine Young katika maelezo yake alikiri kutambua kuwa ujumbe huo ulitumwa na ubalozi wa Marekani nchini na katika ufafanuzi wake alikiri kuwa ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote huku wakitambua kuwa ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hiyo. Aidha,

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo nchini na kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.