Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad (CCM) amechangia shilingi 5,895,000/= kwa ajili ya upauaji wa jengo la wodi ya akina mama katika zahanati ya kijiji cha Zunzuli kata ya Mwenge halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ijumaa Juni 7,2019 katika kijiji cha Zunzuli,kilichohudhuriwa pia na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe.Jasinta Mboneko,mbunge huyo alisema fedha hizo zitatumika kununua mbao na mabati kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya akina mama.


“Baada ya kuona zahanati hii ya Zunzuli haina wodi ya akina mama,nilichokifanya ni kutafuta fedha kwa ajili ya upauaji,namshukuru Mungu wadau wangu wamenishika mkono,nimepata kiasi cha shilingi milioni 5.8 kwa ajili ya kununua mbao na mabati ili wodi hii ya wazazi ambayo wananchi wameijenga hadi kwenye renta ili iweze kupauliwa”,alisema Azza.


“Zahanati hii ya Zunzuli iliyojengwa mwaka 1994 ina chumba kidogo tu chenye vitanda viwili, akina mama wanapokuwa wengi huduma inakuwa tatizo,takwimu zinaonesha zahanati hii inapokea akina mama wanaojifungua kati ya 20 hadi 25 kwa mwezi ndiyo maana nikaona umuhimu wa kuwatafutia fedha za upauaji ili akina mama waweze kupata huduma wanayostahili”,aliongeza mbunge Azza.

Alisema jukumu lake kubwa kama mbunge wa viti maalum na mbunge mwanamke ni kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na hiyoni kuunga mkono kwa vitendo jitihada zinazofanywa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya afya.

Kwa upande wake,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Mhe. Jasinta Mboneko aliwataka wananchi kutumia fedha zilizotolewa na mbunge kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwakumbusha kuwa mstari wa mbele kuchangia shughuli za maendeleo badala ya kusubiri serikali pekee iwaletee maendeleo.

Mboneko pia aliwahamasisha wanawake kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya afya huku akiwasisitiza akina baba kutunza na kukaa vizuri na wake zao badala ya kuwanyanyasa na kupeleka watoto shule badala ya kuwaozesha.

Wa pili kulia ni diwani wa kata ya Mwenge Edward Maganga akimwongoza Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad (wa pili kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe.Jasinta Mboneko (katikati) walipowasili katika zahanati ya Zunzuli Juni 7,2019 . Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Muonekano wa jengo la wodi ya akina mama katika zahanati ya Zunzuli kata ya Mwenge ambapo limefikia kwenye renta na tayari Mbunge amepata fedha kwa ajili ya upauaji.
Mganga mfawidhi Zahanati ya Zunzuli Dkt. Manumi Julius akionesha jengo la zahanati ya Zunzuli.
Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad (CCM) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Zunzuli na kuwaambia amepata fedha kwa ajili ya upauaji wa jengo la zahanati ya akina mama zinawekwa kwenye akaunti ya kijiji.
Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Zunzuli.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe.Jasinta Mboneko akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Zunzuli na kuwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza na wananchi wa kijiji cha Zunzuli.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Mhe. Hoja Mahiba akizungumza kwenye mkutano huo. P.icha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog