Mwanamama mjasiriamali, raia wa Uganda ambaye amezaa watoto wawili na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ amekasirishwa na ‘intavyu’ iliyofanywa na mpenzi wa sasa wa baba watoto wake huyo, Tanasha Donna Oketch na kumpa onyo zito.  Zari alichukizwa na mahojiano ya Tanasha na timu ya Wasafi kwa jumla na kuwataka kuacha kutumia jina lake kwenye mambo yao.

Tanasha ambaye ni raia wa Kenya, wikiendi iliyopita alifanya mahojiano hayo maalum na redio moja jijini Dar kisha kusambaa kwenye kurasa zote za mitandao ya kijamii inayosimamiwa na mastaa walio kwenye Lebo ya Wasafi inayosimamiwa na Diamond au Mondi.

Katika mahojiano hayo, Tanasha alitakiwa kutoa maoni yake juu ya uhusiano mbovu wa mpenzi wake huyo na Zari. Tukumbuke Diamond na Zari wamekuwa kwenye ugomvi mzito wa kurushiana maneno makali mitandaoni huku mwanamama huyo akimtuhumu jamaa huyo kumtelekezea wanaye wawili, Tiffah na Nillan.

Katika hilo, Diamond naye amekuwa akimtuhumu Zari kumzuia kwenda kuwaona watoto wake na kukataa wasifike Tanzania kutoka Afrika Kusini anakoishi nao kwa sasa. Katika maoni yake, Tanasha alifunguka kwamba angependa kukutana na watoto wa Diamond aliozaa na Zari. Tanasha aliwashauri Diamond na Zari kuweka kando tofauti zao kwa manufaa ya watoto wao ili wawalee vizuri.

“Watoto hawana wanachokipata kutokana na kile kinachoendelea kati yao (Diamond na Zari),” alisema Tanasha ambaye ni mtangazaji wa redio moja jijini Mombasa, Kenya. Baada ya mahojiano hayo ndipo Zari akaja juu kupitia ukurasa wake kwenye Stori za Instagram. Zari alifunguka kuwa Wasafi na timu yao waache mara moja kutumia jina lake kwenye mambo yao.

“Hawa Wachafu (kinyume cha Wasafi) wanahitaji kuniacha, kwani hamuwezi kufanya mambo yenu bila kutaja jina langu? “Kwani mimi ni oksijeni mseme hamuwezi kuhema bila mimi?” Alihoji Zari akijibu intavyu hiyo ya Tanasha. Si mara ya kwanza kwa Zari kumuonya Tanasha kwani miezi kadhaa iliyopita alimtaka kuchukua tahadhari juu ya Diamond kwani hachelewi kumuacha solemba.