Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amewasimamisha kazi watumishi watano wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili kupisha uchunguzi dhidi yao.

Watumishi hao waliosimamishwa kazi ni Mhandisi Naomi Adoncome Mcharo, Bw Robert Samson Fundi, Bi Doris Daniel Sendewa, Bw Mohamed Ally Mchemi na Bw Mujuberi Thomas Masatu.

Waziri Hasunga amesema kuwa watumishi hao wamesimamishwa kazi kufuatia taarifa ya awali ya uchunguzi iliyoundwa na ofisi ya Waziri Mkuu kubaini udhaifu wa kiutendaji ndani ya Tume ya Umwagiliaji ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za miradi, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na kukosa umakini katika ujenzi wa Miradi ya Umwagiliaji.

Alisema kuwa watumishi hao watano wataungana na watumishi wengine waliosimamishwa kazi hivi karibuni na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa ambao ni Wakurugenzi saba wa Tume ya Umwagiliaji akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo.