Wakutwa na Kilo 200 za nyama ya Kiboko, yupo Mzee wa miaka 70, wafikishwa kortini
Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa mawili ikiwemo ya kujihusisha na nyara za serikali na kukutwa na nyama ya Kiboko yenye uzito wa Kilo 200 ikiwa na thamani ya Sh.Mil 3.44.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 44 ya mwaka 2019, washitakiwa ni Ayoub Kayanda mkazi wa Karakata Mji Mpya (70), Jumanne Sia (47), mkazi wa Msolwa Mkuranga, Said Lwambo (49) na Ally Nongu (54), Wakazi wa Mbezi Mkuranga.

Washitakiwa wamesomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwezire na wakili wa Serikali Saada Mohammed ambaye amedai kuwa washitakiwa walitenda makosa yao kwa nyakati tofauti.

Katika kosa la kwanza la kukutwa na nyara za serikali kwa pamoja wanadaiwa  Mei 9, 2019 maeneo ya Nzasa wilaya ya Temeke walikutwa na Kilo 200 za nyama ya Kiboko ikiwa na thamani Milioni 3.44 huku wakiwa hawana kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Kosa jingine ni kujihusisha na nyara za serikali ambapo kwa pamoja wanadaiwa kati ya Mei 7 na 9, 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na mkoa wa Pwani walikubali kusafirisha Kilo 200 za Nyama ya Kiboko ikiwa na thamani ya Mil.3.44 bila kuwa na kibali.

Wakili Saada amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba ahirisho la kesi. Washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote baada ya kuibuka hoja kama Mahakama hiyo inapaswa kusikiliza kesi hiyo ama lah ambapo kesi imeahirishwa hadi Mei 31, 2019 ili Hakimu atoe uamuzi, washitakiwa wamerudishwa rumande.