Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika, Mheshimiwa Stephen Masele akiwa ofisini kwake katika Makao Makuu ya Bunge la Afrika, Midrand, Johannesburg, Afrika Kusini akizungumza na Ujumbe wa wabunge kutoka Bunge la Uganda waliotembelea Bunge la Afrika leo Mei 14,2019. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Kushoto ni Mhe. Masele akizungumza na Ujumbe wa wabunge kutoka Bunge la Uganda (kulia) waliotembelea Bunge la Afrika.
Wabunge wa Bunge la Uganda wakimsikiliza Mhe. Masele.
Kiongozi wa Ujumbe huo wa wabunge kutoka Uganda Mhe. Ongalo Obote Kenneth akielezea lengo la ziara yao kutembelea Bunge la Afrika.
Picha ya pamoja,Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika,Mheshimiwa Stephen Masele na wabunge wa bunge la Uganda.
Mbunge kutoka Uganda, Mhe. Mugoya Kyawa (kulia) akiteta jambo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika, Mhe. Stephen Masele.
---
---
Wabunge wa Bunge la Uganda wametembelea Bunge la Afrika ‘Pan - African Parliament’ katika makao yake makuu Jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini ili kujifunza namna bunge hilo linavyofanya kazi.
Ujumbe huo wa wabunge nane kutoka Uganda ukiongozwa na Mheshimiwa,Ongalo Obote Kenneth umepokelewa leo Jumanne Mei,14 2019 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika,Mheshimiwa Stephen Masele ambaye anatoka Tanzania,Kanda ya Mashariki ya Afrika.
Mhe. Kenneth alisema lengo la kufika katika Bunge la Afrika ambalo wabunge wake wanaendelea na Mkutano wa pili wa kawaida wa bunge la tano la tano ni kujifunza namna bunge hilo linavyofanya kazi.
“Tumefurahi kufika hapa kuona na kujifunza mambo kadha wa kadha kuhusu Bunge la Afrika, ikiwemo historia yake,muundo wake na namna wanavyoendesha shughuli zao na kuzungumzia masuala ya Afrika,kwa kweli bunge hili ni imara kupitia viongozi wake akiwemo,Mheshimiwa Masele ambaye ni kijana lakini ana uwezo mkubwa wa kuongoza taasisi hiyo kubwa Afrika”,alisema Mhe. Kenneth.
Kwa upande wake, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika, Mhe. Stephen Masele amewapongeza wabunge hao kwa kuona umuhimu wa kutembelea bunge hilo kujifunza kuhusu bunge na siasa za Afrika.
“Nimefurahi kupokea ujumbe wa wabunge wa bunge la Uganda wanaotoka katika kamati mbalimbali,mmejionea jinsi tunavyoendesha shughuli za bunge la Afrika,wamefahamu kuhusu historia ya bunge,historia ya Umoja wa Afrika (AU),ukombozi Afrika na mambo mengine”,alisema Mhe. Masele.
“Bunge la Afrika lina wabunge kutoka nchi mbalimbali barani Afrika,wenye tamaduni na lugha tofauti tofauti,ninaamini kwa siku zote mtakazokuwa hapa bungeni,mtafaidika vya kutosha kuhusu siasa za Afrika”,aliongeza Mhe. Masele.