Na Shamimu Nyaki -WHUSM
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza amevielekeza Vyama na Mashirikisho ya Michezo nchini kuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya afya  na kinga  kwa wanamichezo  ili kulinda afya za wanamichezo hao kabla, wakati na baada ya mIchezo.

 Shonza ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma alipokua akijibu swali la msingi la Mhe. Haji Khamis Mbunge wa Nugwi aliyetaka kufahamu Serikali kupitia Vyama vya Michezo imeweka utaratibu gani wa kuhakikisha upimaji wa afya za wanamichezo linalopewa kipaumbele.
Naibu Waziri ameeleza kuwa Kitengo cha Kinga na Tiba kilichopo katika Wizara yake kwa kushirikiana na Chama cha madaktari wa Michezo nchini (TASMA) kinafanya kazi kubwa ya kutoa elimu pamoja na huduma ya afya kwa wanamichezo.

"Kitengo cha Kinga na Tiba cha Wizara jukumu lake ni kutoa elimu ya afya kwa wanamichezo pamoja na kutoa huduma ya upimaji wa afya kwa wanamichezo kila wanaposhiriki michezo au mashindano mbalimbali, hivyo vyama vya michezo na mashirikisho vinapaswa kuzingatia maelekezo hayo," alisema Mhe. Shonza.

Aidha Naibu Waziri huyo amongeza kuwa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 sehemu ya 10.1 imeelekeza kuwa ni lazima mchezaji achunguzwe afya yake na kuwekewa kumbukumbu zote za kiafya kwa kipindi chote anapokuwa kambini na ahudumiwe na kuwekewa kumbukumbu zote za kiafya kwa kipindi chote anapokuwa kambini na ahudumiwe na Daktari mwenye taaluma ya tiba ya wanamichezo.

Vilevile  Shonza amesema kuwa Wizara iko tayari kutoa ushirikiano katika jitihada za kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuimarisha afya za wanamichezo muda wote wanapokuwa uwanjani katika mazoezi au mashindano mbalimbali.
Hata hivyo Naibu Waziri Shonza alipojibu swali la nyongeza la Mhe.Sophia Mwakagenda aliyeuliza ni lini mabondia watapatiwa Bima ya Afya alieleza kuwa Shirikisho la ngumi hapa nchini tayari limeelekezwa kuwa na utaratibu wa kuwatafutia Bima mabondia hao.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akijibu swali wakati wa kikao cha 40 cha Bunge leo jijini Dodoma.