Viongozi wa Umoja wa Ulaya wapo mjini Brussels Ubelgiji, kwaajili ya mchakato wa kuwateua wakuu wapya watakaopewa nyadhifa za kusimamia taasisi mbalimbali za umoja huo.
Hilo linajiri baada ya uchaguzi wa bunge la Ulaya ambao, ulivitikisa vyama vikuu.
Kazi kubwa itakuwa kumteua atakayekuwa rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya.
Rais wa halmashauri hiyo huwa na mamlaka makubwa na huhudumu kwa miaka mitano.
Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Jean-Claude Junker.
Tayari kuna mabishano kuhusu nani anapaswa kushikilia wadhifa huo.
Wafuasi wa vyama vya kihafidhina vinavyounga mkono Umoja wa Ulaya EPP wanadai mgombea wao Manfred Weber ndie anaestahiki kukabidhiwa wadhifa wa mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anapinga wazo la kwamba mwenye kuongoza orodha ya wagombea ndie anaebidi akabidhiwe wadhifa huo.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema muungano anaoongoza, unaunga mkono wazo kuwa kiongozi wa halmashauri hiyo anapaswa kuwa mwanasiasa aliyewania kiti hicho.