Baadhi ya Viongozi Wa Dini Mkoani Arusha Wahitimu Mafunzo Ya Usalama Barabarani

Na Vero Ignatus, Arusha.

Baadhi ya Viongozi mbalimbali wa dini kutoka katika baadhi ya makanisa Mkoani Arusha wamehitimu mafunzo ya udereva lengo likiwa ni kudhibiti ajali zinazosababisha vifo na majeruhi,ambapo yametolewa na Chuo cha Wide Institute of Driving.

Faustine Matina ni Mkufunzi wa Chuo hicho amesema kuwa mafunzo hayo ya Usalama barabarabi yamefanyika kwa umakini mkumbwa kwa viongozi hao ili waweze kuwa mabalozi wa masuala ya usalama barabarani na kuokoa maisha ya watu.

Viongozi hao wa dini wamehitimu mafunzo hayo na kupatiwa vyeti hivyo kukidhi matakwa ya serikali ya kuwataka madereva kuwa na vyeti vya shule ya udereva pamoja na leseni kama vigezo muhimu kwa madereva.

Joseph Bukombe ni Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha ambapo amewataka viongozi hao wa dini kuhubiri masuala ya usalama barabarani katika makanisa yao ili kuokoa maisha ya waumini wao ambao wengi ni madereva.

“Nawaomba msikae kimya mkazungumze huko makanisani badala ya kusema nendeni kwa amani muwaambie kuwa wasisahau kufunga mkanda wanapokua kwenye magari yao kwa kufanya hivyo tutaokoa maisha yao” Alisema Bukombe.

Aidha Bukombe amewataka pia Wanasiasa kuwaambia ukweli madereva bodaboda kutii sheria za usalama barabarani badala ya kuwatetea bila kuwaambia ukweli kwani ajali nyingi zinazotokea mkoa wa Arusha zinasababishwa na bodaboda.

Namsemba Mwakatobe ni muwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ambaye ni Mrakibu wa polisi Makao Makuu ya polisi Arusha amesema kuwa jeshi la polisi litashirikiana na viongozi wa dini katika kutatua changamoto za usalama barabarani sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.

Askofu Stanley Hotay ni Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoani Arusha amekiri kuwa mafunzo hayo yatawasaidia Viongozi hao kuwa na uelewa mkubwa na kujifunza vitu vingi ambavyo walikua hawavijui kuhusu usalama barabarani.