*Majaribio yaanza kufanyika, Mhandisi Kamwele afurahishwa na kasi aipongeza TAA

* Ujenzi daraja la Salender wakamilika kwa asilimia 9.5, ujenzi kuanza mwisho wa mwezi huu

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaack Kamwele amefanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo jipya  la 4  la abiria (Terminal 3) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Julius Nyerere (JNIA) leo jijini Dar es Salaam na kuonesha kuridhishwa na usimamizi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamwele amesema kuwa kasi ya ujenzi huo ni nzuri na hadi sasa uwanja umekamilika na upo katika majaribio na utakabidhiwa rasmi tarehe 29 mwezi huu badala ya tarehe 31 na hiyo ni baada ya uwanja huo kukamilika kwa asilimia kubwa.

Amesema kuwa majaribio kwa ajili ya uwanja huo wa terminal 3 unaendelea huku akiwahimiza wazawa kutumia fursa ya kutumia nafasi maalumu zilizowekwa kwa ajili ya kuuza chakula (canteen) ili waweze kujiongezea kipato.

Aidha ameipongeza Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kwa kusimami vyema mradi huo na amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kuleta maendeleo yenye tija kwa kuwa kupitia uwanja huo watalii wengi wanatarajia kuingia nchini huku akieleza kuwa hali ya ulinzi uwanjani hapo ni salama kwa kila mmoja atakaye kuwepo uwanjani hapo.

Kuhusiana na ujenzi wa daraja la Salender Kamwele amesema kuwa kasi inaenda vyema na barabara ya muda inajengwa na mwisho wa mwezi huu ujenzi rasmi utaanza rasmi.

Amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo lenye mita 1030 umekamilika kwa asilimia 9.5 na tayari mitambo na nguzo zimewasili kwa ajili ya kazi hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini Mhandisi. Julius Ndyamukama amesema kuwa uwanja wa Terminal 3  una uwezo wa kubeba zaidi ya watu milioni 6 kwa mwaka, kupaki ndege kubwa 13 umekamilika na kazi za majaribio zinaendelea ikiwemo kufunga mitambo kutoka mamlaka za  uhamiaji, mabenki, shirika la simu la TTCL na wadau wakubwa katika uwanja huo.

Amesema kuwa zaidi wa wananchi 2900 ambao ni sawa na asilimia 70 wamenufaika na ajira kupitia mradi huo na ameipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kasi katika usimamizi wa miradi ya kimaendeleo na kuahidi kuendelea kutekeleza miradi ya namna hiyo kwa wakati.

Tafiti zinaonesha  kuwa Uwanja wa Terminal 1 una uwezo wa kubeba watu laki tano kwa mwaka, Terminal 2 una uwezo wa kubeba watu zaidi ya milioni mbili na nusu  kwa mwaka na ujenzi wa uwanja wa terminal 3 unataraji  kubeba watu zaidi ya milioni 6 kwa mwaka na umekuja baada uwanja wa terminal 2 kuzidiwa na idadi kubwa ya watu na hii ni kutokana na kukua kwa uchumi na shughuli za kitalii ambapo watu wengi hutumia usafiri wa anga.

Mradi huo wa ujenzi wa uwanja wa terminal 3 umewekezwa hadi mwaka 2035 kimatumizi huku viwanja vingine 9 vikitarajiwa kujengwa katika Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Ruvuma na Mara.
 Msimamizi wa mradi kutoka TANROAD Mhandisi. Burton Komba (kulia) akitoa maelezo kwa waziri Kamwele kuhusiana na namna uwanja huo utakavyofanya kazi,  leo jijini Dar es Salaam
 Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa terminal 3 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa  Julius Nyerere ambapo amesema kuwa kasi na ubora wa ujenzi wa uwanja huo inaridhisha na majaribio yanaendelea, leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele akizungumza na watendaji na wasimamizi wa mradi huo, kulia na msimamizi wa mradi kutoka TANROAD Mhandisi Burton Komba na katikati ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini Mhandisi Julius Ndyamukama, leo jijini Dar es Salaam.