Bukoba na Allawi Kaboyo.
Umoja wa mashabiki wa timu ya soka ya Kagera Sugar inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara wameiandalia timu hiyo futari iliyowajumuisha wachezaji wote wa timu hiyo,benchi la ufundi, viongozi wa timu pamoja na mashabiki ikiwa ni ishara ya kuonesha umoja na upendo kwa timu yao.
Futari hiyo iliandaliwa jana tarehe 16 mwezi machi mwaka huu katika ukumbi wa Red Cross Bukoba mkoani Kagera na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kiserikali na dini katika kuonesha mshikamano baina ya mashabiki na timu.
Akiongea mmoja wa viongozi wa umoja wa mashabiki ambaye ni katibu wa jumuiya hiyo ndugu Alex Xavery aliutaka uongozi wa timu ya Kagera sugar kuonesha ushirikiano na mashabiki ili kuweza kuijenga timu lakini pia kuwafanya mashabiki kuwa karibu zaidi na timu yao.
Katibu huyo aliongeza kuwa timu kwa sasa ina hali mbaya katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara kutokana na kutofanya vizuri katika msimu huu ambapo alimuomba mwalimu wa timu hiyo Meck Maxime kuwa na malengo ya kuchukua taji hilo kwa msimu ujao endapo wataweza kubakia kwenye ligi kutokana na nafasi ya timu iliyopo kwa sasa.
“Timu yetu tunajua hali iliyonayo na sasa tunamuomba mungu tubakie kwenye ligi, tukuombe mwalimu uanze kuwa na malengo ya kuchukua ubingwa msimu ujao. Zipo tetesi za kuwa mashabiki tukiwa na nguvu tutaichukua timu irudi kwa wananchi mimic niseme tu hilo sio lengo letu kwanza tunajua hatuna uwezo wa kuiendesha timu,ila tunachotaka kwenu ni ushirikiano na kitu kikubwa ambayo mnaweza kutulipa ninyi kama benchi la ufundi na wachezaji ni matokeo mazuri.” Alisema Alex.
Alex alisisitiza kuwa wao kama wachezaji wa 12 ambao hukaa nje ya uwanja kwaajili ya kuwahamasisha wachezaji hujisikia vibaya pale mchango wao unaposhindwa kuthaminiwa nap engine kuonekana wanajipendekeza.
Kwa upande wake kocha mkuu wa timu hiyo Meck Maxime aliwaomba radhi mashabiki hao kwa mwenendo mbaya wa timu kwa sasa katika msimu huu ambapo alisema kufungwa ni sehemu ya mchezo na kukili mbele ya mashabiki hao kuwa hali ya timu kwa sasa sio nzuri na kuomba waombewe dua ili waweze kubakia katika ligi kuu Tanzania Bara.
Maxime alisema kuwa mashabiki wasipende sana kulalamikia uongozi bila hata kuwauliza uongozi husika juu ya jambo linalowakera ambapo aliuueleza umma uliojitokeza katika futari hiyo kuwa wao wanawapenda sana mashabiki wao.
“Ninachojua mashabiki mnapenda kuiona timu ikifanya vizuri na hatimaye kuleta matokeo yaliyo mazuri, lakini tambueni mchezo una kufunga,kufungwa na kutoka suruhu hivyo tunaomba matokeo yote ambayo timu itayapata tuyapokee sote isiwe timu ikifungwa ni timu ya kocha lakini ikishinda ni yetu sote.” Alisema Maxime.
Aidha Maxime alisema kuwa wamefurahishwa na upendo ulioneshwa na umoja wa mashabiki kwa kuwaandalia Futari na kuongeza kuwa kwa shabiki yeyote atakayeona jambo ambalo anahisi hakulielewa basi asianze kulalamika awafate viongozi watamueleza juu ya jambo hilo.
Timu ya Kagera Sugar jana ilicheza mchezo wake wa 36 wa ligi kuu Tanzania Bara na timu ya soka ya Stand Utd kutoka Mkoani Shinyanga katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na kukubali kichapo kitakatifu cha goli 3 kwa 1(3-1) na kuifanya timu hiyo kushuka kutoka nafasi ya 13 hadi nafasi ya 15 ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa imecheza michezo 36 ikiwa na alama 43 huku vinala wa ligi hiyo wakiwa ni mabingwa watetezi wenye alama 85 baada ya kucheza michezo 34.