Maafisa waandamizi na watendaji wa Idara ya Uhamiaji wametakiwa kuwa makini katika suala zima la ulinzi pamoja na usalama wa mipaka ya nchi ili kuliepusha Taifa kuvamiwa na wageni wasiokuwa waaminifu.

Kufanya hivyo kutalisaidia Taifa pamoja na wakazi wake kuendelea kuishi katika mazingira salama muda wote na kufanya kazi zao bila ya hofu.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd.Shaaban Seif Mohamed alieleza hayo wakati akizungumza na maafisa na watendaji wa idara ya Uhamiaji katika ukumbi wa Ofisi hizo zilizopo Kilamani Mjini Zanzibar.

Alisema Idara ya Uhamiaji ni taasisi muhimu na nyeti katika kuhakikisha mipaka ya nchi inakuwa salama hivyo kuna haja ya kufanya Doria au ukaguzi kwa uwaangalifu katika mipaka ya Nchi kavu na baharini ili kuweka udhibiti wa wahamiaji haramu,na kufanya uvamizi.

“Nitoe mfano kuna changamoto ya bandari bubu zinazopokea wageni bila ya kuwepo maafisa kutoka idara ya Uhamiaji jambo ambalo ni hatari na linafaa kuachwa mara moja”. Alisema Katibu Mkuu Shaaban.

Nd. Shaaban alifahamisha kwamba suala la ulinzi wa mipaka katika ndani ya nchi linahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya idara hiyo na wananchi wake sambamba na watendaji kutoka Serikali Kuu.

Akijibu baadhi ya Changamoto zinazoikabili idara hiyo Katibu Mkuu alisema viongozi wanaosimamia majukumu mbali mbali wanapaswa kuzisemea Changamoto hizo kwa viongozi wanaohusika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na aliwahidi maafisa hao kwa yale yanayoweza kupatiwa ufumbuzi Serikali itayachukulia hatua.

Akisoma taarifa ya Idara ya Uhamiaji Naibu Kamishna utawala na Fedha Ali Suleiman Nassor alimuelezea Katibu Mkuu Shaaban kuwa idara ya uhamiaji Zanzibar imefanikisha kuwakamata wageni 205 na kuchukuliwa hatuwa za kisheria ambapo kati yao 26 waliondoshwa nchini na 109 walilipia vibali,15 walishtakiwa Mahakamani ,21 waliachiwa Huru baada ya uchunguzi na wageni 34 bado uchunguzi unaendelea .

Naibu Kamishna Ali alieleza idara ua Uhamiaji katika Kuimarisha Ulinzi na Usalama imewatambua na kuwaoredhesha wahamiaji walowezi 1, 281, Unguja na Pemba kati ya hao 668 wameshasajiliwa .

Vile vile alieleza katika suala zima la utoaji wa vibali , Idara imetoa jumla ya vibali 1,116 kwa wageni kwa shughuli mbali mbali ikijumuisha vibali 143 vya daraja A, 536 vya daraja B, 437 vya daraja C, 225 hati za ufuasi na 250 hati za msamaha.

Alisema katika mwaka wa Fedha 2018/2019 Idara ilipangiwa kukusanya Shillingi 30,001,727,413/- kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Machi 2019 ambapo hadi sasa imekusanya Jumla ya Shillingi 26,104,134, 382.42/- sawa na asilimia 87% ya malengo ya Makusanyo yote.

Akigusia Changamoto zinazoikabili Idara hiyo Naibu Kamishna alizitaja Changamoto hizo ikiwemo Ufinyu wa Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi ,kukwama kwa utaratibu wa kumalizia upatikanaji wa eneo la Kitogani kwa ajili ya Ujenzi wa eneo la Chuo cha Uhamiaji pamoja na ukosefu wa boti kwa ajili ya kufanyia doria.

Wakichangia katika Kikao hicho Maafisa wamemtaka Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzitembelea Afisi nyengine za Wilaya Unguja na Pemba ili kujionea hali halisi ya Mazingira ya Kazi .
 Naibu Kamishna utawala na Fedha Ali Suleiman Nassor Kushoto akimpokea Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed aliyefika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Zanzibar kuzungumza na Makamanda na Watendaji wa Jeshi hilo.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed akitia saini kitabu cha Wageni alipofika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Zanzibar kuzungumza na Makamanda.
 Naibu Kamishna utawala na Fedha wa Uhamiaji Zanzibar Ali Suleiman Nassor akitoa Taarifa ya uwajibikaji wa Jeshi hilo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif Mohamed alipofika kuzungumza nao.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Ndugu Shaaban Seif akizungumza na Makamanda na Watendaji wa Jeshi la Uhamiaji Makao Makuu yao Kilimani Mjini Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.