TUZO za Mo Awards zilizoasisiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji zinatolewa leo Alhamisi ukiwa ni msimu wake wa pili. Tukio hilo la aina yake litafanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency na zitatolewa tuzo 12 kwa kikosi hicho cha Mabingwa wa Ligi Kuu Bara.



Hii itakuwa ni mara ya pili kwa tuzo hizo kutolewa baada ya mara ya kwanza mwaka jana.

Msimu huu tuzo hizo zitakuwa na mabadiliko tofauti na msimu uliopita baada ya vipengele kadhaa kuongezwa.


Tuzo hizo zitakuwa katika vipengele 12 ambavyo ni mchezaji bora wa mwaka, golikipa bora wa mwaka, goli bora la mwaka, beki bora wa mwaka, kiungo bora wa mwaka na mshambuliaji bora wa mwaka mchezaji mwenye umri mdogo, mchezaji bora wa kike na nyingine.



Hata hivyo tuzo hizo zilikuwa zinapigiwa kura katika kurasa tofauti za mitandao ya kijamii ya klabu ya Simba. Wachezaji ambao walipata tuzo hizo msimu uliopita ni pamoja na Aisha Manula, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi kwa Simba Queens alikuwa Zainabu Rashid. Kwa upande wake, Mohammed Dewji amesema kuwa tuzo za mwaka huu zitakuwa na hadhi kubwa zaidi tofauti ya zile za mwaka uliopita kutokana na maandalizi ambayo yamefanyika.